Category: Jamvi la Kiswahili

  •  MFANYAKAZI WA NYUMBANI

    {Picha kwa hisani ya Conde Nast Travelers}

     

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com}

    Kwa miaka mingi sasa watu wengi wamezoea kuwaajiri wafanyakazi wa ndani ili kuwasaidia kazi. Wafanyakazi hawa wa nyumbani ni wasaidizi au wakelezaji wa kazi zote za nyumbani ikiwemo kufua, kupika, kufanya usafi wa nyumba na mazingira, kuosha vyombo na baadhi ya kazi zingine nyingi wanazopewa na waajiri wao. Mbali na kazi hizo, wafanya kazi wengi hupewa kazi ya kulea watoto endepo mama au wazazi ameenda kazini, au kama wanataka kuendelea na shughuli zingine.

    Kabla sijaelezea jinsi baadhi ya mambo ya ajabu ambayo wafanyakazi huwafanyia watoto, tutaanza na jinsi wafanyakazi hawa huteswa katika baadhi ya sehemu wanapoajiriwa. Kwanza kabisa, mtu anapomwajiri mfanya kazi anatakiwa ahakikishe kua hamtesi wala kumyanyasa kwa namna yoyote ile, na badala yake anatakiwa akumbuke haki yake. Hii ni kwasababu wafanyakazi hawa ndio walinzi wa nyumba na wana uwezo wa kuiangamiza au kuistawisha familia.

    Wafanyakazi hawa hupitia changamoto nyingi kama vile kunyimwa chakula na mavazi mazuri, kupigwa, kutopewa mahali pazuri pa kulala, kufanyishwa kazi nyingi nje ya uwezo wao na hata kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao. Waajiri hawa husahau mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi hawa ingawa bado wanawahitaji.

    Kumetokea kesi nyingi ya wafanyakazi hawa wa ndani wa kike, kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao wakiume na hii imeleta migogoro katika familia nyingi na kusababisha kuvunjika kwa ndoa. Wengi wao wakitoa malalamiko, hawaaminiwi kwa sababu wanalaumiwa kuwa sababu ya kilichowapata. Unapata mume au baba mwenye nyumba ana familia ya pili na mfanya kazi wa ndani.

    Kuna baadhi ya haki ambazo wafanya kazi wanastahili kupewa ikiwemo likizo kwa sababu wengi wao hufanya kila siku bila kupumzika na inawalazimu kusingizia kuumwa ili waweze kupumzika au kuenda kuwasalimia wazazi wao nyumbani. Wanatakiwa pia walipwe mishahara yao kamili na kwa wakati, na kuhakikisha ulinzi wa afya na usalama wao.

    Kati ya hayo machache kuhusu haki na usalama wa wafanya kazi wa nyumbani, tutaangazia vitendo vya ajabu vinayofanywa na wafanyakazi hawa katika familia tofauti haswa kwa watoto wanaoachiwa kuwalea.

    Wafanya kazi hawa wa ndani hushikwa wakiwadhulumu, kushiriki kingono na watoto wa waajiri wao na wakati mwingine kuwapiga na kuwaumiza watoto hawa. Inasikitisha kwa sababu watoto hawa hushindwa kutoa mashtaka kwa wazazi kutokana na umri wao kua mdogo na sababu nyingine ni vitisho wanavyopewa. Wafanya kazi wengi hunyanyasa watoto kwa sababu ya kukosa subira pindi mtoto anapokataa kula, kulala au kumsikiliza.

    Wazazi hawa hugundua hizi shida na mateso watoto wao wanayoyapitia baadae sana wakati mtoto ashaharibiwa kupitiliza. Kesi nyingi zimetolewa dhidi ya wafanya kazi wa nyumbani lakini bado idadi inatia shaka. Wazazi wanatakiwa wahakikishe wanawaajiri wafanyakazi wazuri waliobobea ili watoto wao wawe kwenye mikono salama, kwa sababu wakati mwingi wapo kazini na wanachelewa kurudi hivyo hawajui kinachoendelea nyumbani. Wakati mwingine wazazi hawa wanashauriwa angalau kukaa na mtoto kwa muda mwingi na sio tu kutokomea kazini ilhali mtoto hayupo salama.

    Kutokana na uzoefu wa kuwaachia wafanya kazi wa nyumbani watoto ili wawalee, hamna namna nyingine bali kuhakikisha wafanya kazi hawa ni wa kuaminika na wenye utu na huruma.

     

  •    AFYA YA AKILI

    (Photo courtesy of uCheck Blog)

    Na: Gertrude Prosper

    getrude2003@gmail.com 

    Afya ya kiakili ni hali ya kuwa sawa kiakili, kisaikolojia na kuwa na mawazo chanya. Afya ya kiakili ni muhimu kwa sababu inahusiana na jinsi akili ya mtu inavyofanya kazi.

    Miaka inavyozidi kuenda, afya ya kiakili inaharibiwa na hivyo kusababisha watu kupata matatizo ya kiakili. Matatizo haya ya kiakili hayachagui jinsia, aina ya kazi mtu anayofanya wala umri, mtu yeyote anaweza kupata, sanasana vijana ndio wanaonekana kuathirka kwa asilimia kubwa. Watu wengi wamezoea kupuuzia kuhusu afya ya akili zao na hii imewafanya kugundua kua wanamatatizo ya kiafya baadae wakati wameshachelewa.

    Mwelekeo wa matatizo ya afya ya kiakili duniani unazidi kutia shaka kutokana na idadi ya watu inavyozidi kuongezeka. Wataalamu wa afya ya kiakili wanatakiwa waongeze bidii ili kutoa matibabu na huduma dhidi ya vyanzo vya matatizo ya akili. Sio waatalamu tu, hata ndugu, jamaa na marafiki wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa watu hawa.

    Vyanzo au vichochezi vya matatizo ya kiakili ikiwemo ukatili wa kingono/ kijinsia, uonevu, unanyasaji, unyanyapaa, ubaguzi, ugumu wa maisha na ukiukaji wa haki za binadamu. Vyote hivi vinaweza kumsababishia mtu kupata matatizo ya afya ya kiakili. Kando na hayo, huzuni, kusononeka, hofu, woga na hasira ya kila wakati vanaweza kua ni vyanzo vya matatizo ya akili.

    Vyanzo wengine ni migogoro katika familia ikiwemo wazazi au walezi kugombana mbele ya watoto, kuwapiga watoto wao au kutumia lugha isiyofaa kwa watoto. Hii inaleta matatizo ya kisaikolojia kwa watoto. Wazazi au walezi wanatakiwa kua mifano bora kwa watoto kwasababu hawa ndio vijana watakaokuja kuteseka kiakili baadae. Wazazi wanatakiwa wahakikishe kuwa wao ndio mstari wa mbele kuwalinda na kuwajengea watoto mienendo na maadili inayofaa katika maisha. Vijana ndio taifa la kesho.

    Athari za kutoshughulikia matatizo ya afya ya kiakili husababisha mambo makubwa kama vile kuleta misongo ya mawazo, kiwewe, kuwalazimu watu kujiua na matumizi ya pombe na mihadarati.

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwepo kwa ripoti nyingi za mauaji kutokana matatizo ya kiakili, na bara la Afrika likiwa linaongoza kuliko mabara mengine duniani. Takriban zaidi ya watu 10 kati ya 100,000 hufa barani Afrika, ambayo ni zaidi ya wastani wa kimataifa. WHO imesema kuwa Afrika ina uhaba wa matibabu na huduma wa magonjwa ya afya ya kiakili, hii ni kutokana na imani potofu zinazowafanya watu kupuuzia magonjwa haya. Watu hawa wanapokosa msaada wanalazimika kujiua au kufanya matendo ya kujiumiza.

    Mtu anapoishi kwa huzuni mwingi, kukosa usingizi, kua na mshtuko, mawazo mabaya, upweke, dhiki, wasiwasi au kusikitika kushusu maisha, ni vizuri kutafuta msaada mapema kabla ya kufanya mambo ya kujiumiza.

    Matibabu ya kiakili na huduma ni pamoja na kuzungumza au kuwasiliana na watu unaowaamini ikiwemo marafiki, familia, wahudumu wa afya, na wakijamii. Mawasiliano kwa kawaida ni kwa ajjili ya kupashana au kubadilishana habari, hisia, maoni au mawazo kwa kutumia maneno, maandishi au ishara.  Watu wengi hushindwa kuwasilisha hisia zao kwa muda unaofaa na hii huwasababishia madhara mengi ikiwemo afya ya kiakili. Wengi wao huona ni vigumu kujielezea kwa wengine kutokana na aibu au kutotaka kuonekana wadhaifu. Utayari wa kuzungumza ili kutafuta suluhisho ni hatua muhimu sana, kwasababu inaweza kumsaidia mtu kuepuka kujiua au kupata misongo ya mawazo.

    Ni sawa kutokua sawa, hauko pekee yako. Tafuta msaada mapema.

  • MGENI KIPOFU

    (Picha kwa hisani ya MuseumNext)

     

    Na Abdul S. Shaban

     

    Tazama bila ya hofu, hapo ndipo utaona,
    Alosema muongofu, alitazama kwa kina,
    Pasinapo hitilafu, mimi naye naungana,
    Kuwa mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Mgeni huwa kipofu, hata kama anaona,
    Vitu vyenye upotofu, hasemi atauchuna,
    Huwa anaudhohofu, mjuvi kuonekana,
    Kweli mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Hata aone mnofu, nayo pilau imefana
    Huku njaa takatifu, mgeni imembana,
    Kusema ni ualifu, japo aona bayana,
    Haki mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Mwisho ninawaarifu, wa juzi, leo na jana,
    Muone na msadifu, wala hamtabishana,
    Zaidi utamsifu, mjumbe wake Rabbana,
    Haki mgeni kipofu, hata kama anaona.

  • MAONYESHO YA NANENANE

    (Picha kwa hisani ya Tanzania Agricultural Development Bank)

     

    Na Gertrude Prosper

    Nane Nane ni likizo ya umma nchini Tanzania inayosheherekewa tarehe 8 Agosti, kila mwaka. Ni siku ya maonyesho ya kilimo ambapo wakulima wote nchini wanafanya maonyesho yao ya mazao, mifugo, dawa, na bidhaa katika kanda mbalimbali.

    Leo, Agosti 8 2022 ni kilele cha maonyesho ya nanenane ambapo viongozi pamoja na wananchi wanatembelea mabanda tofauti kujionea mbinu mbalimbali za kilimo bora, uvuvi na mifugo. Wajuzi, wajasiriamali na wataalamu wapo kuadhimisha siku hii kwa kuonyesha bidhaa zao na virutubisho mbalimabli vya mifugo mfano kuku, nyuki, nguruwe na ng’ombe. Wakulima pia wanauza bidhaa kama mashine, dawa, wanatoa elimu na bima ya mazao shambani.

    Siku hii ni muhimu kwasababu inawapa watu fursa ya kuonyesha teknolojia mpya na maendeleo katika kilimo, na kujua zaidi kuhusu uvuvi na ufugaji wa wanyama tofauti. Inawapa watu pia elimu, ujuzi na njia mbalimbali ya kufanya kilimo bora ili kupata mazao mengi ya chakula na biashara. Hii inaongeza vyakula nchini na mapato kwa kuuza nje katika nchi mbalimabli.

    Heri ya Sikukuu ya Nanenane

  • Penzi Halijaribiwi, Utanaswa Unasike.

    (Picha kwa hisani ya The Economic Times)

    Na Abdul Shaban

     

    Mapenzi ya siku hizi, ni ya nipe ndo nikupe,

    Tena ya tele mapozi, kadhalika na mapepe,

    Sipo jali tawa chizi, ujipake na matope,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Penzi halina mjuzi,  nina kwambia peupe,

    panga yako mamuzi, mabaya uje utupe,

    ya sikutoke machozi, yakalovya zako hope,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Mapenzi toka awali, yaliwashinda wa kale,

    Usijione mkali, utarudi na tandale,

    Samsoni nguvu kali, alinaswa palepale,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Ukijifanya bahili, kutosikia wavyele,

    Utashikika pahali, upige zako kelele,

    Kusifiwa ni muhali, huwezi kusonga mbele,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Kujipiga na kifua, eti wewe umakini,

    Utakuja kujutia, ushindwe na kibaini,

    Utalia na dunia, uhame nako nyumbani,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Mwisho nikimalizia, kwa huu wangu waraka,

    Polepole kuanzia, sikuwa nayo haraka,

    Nadhani mumesikia, madada na kina kaka,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

  • Nakusifia

    (Picha kwa hisani ya WBUR)

    Na Abdul Shaban

    Mke ninakusifia,
    Mzuri umetulia,
    Na wala sitojutia,
    Kifua nakitanua.

    Nakupongeza kwa hili,
    Nyumbani nikiwasili,
    Moyo wangu huwa tuli,
    Hali unanijulia.

    Nilipanga mikakakati,
    Masijidi nikaketi,
    Dua pia na swalati,
    Nikamuomba jalia.

    Nikataraji mazuri,
    Mwenye dini ndo mzuri,
    Mola akanitabiri,
    Wewe ndo ukanijia.

    Sitara unatimiza,
    Mazuri wanihimiza,
    Kikosea wanijuza,
    Toba nije kutubia.

    Wanihimiza kwakweli,
    Nichume yalo halali,
    Adhabu zake Jalali,
    Kwangu unanihofia.

    Hongera we mke wangu,
    Wanilelea wanangu,
    Malezi yaso machungu,
    Mola wao kumjua.

    Naomba kwake manani,
    Tusitengane ndoani,
    Wenye shari maishani,
    Wacheze pata potea.

    Zimekujaa swifati,
    Mahabuba habibati,
    Nitazimaliza beti,
    Sifa hazitoishia.

    Utenzi naumaliza,
    Machozi nabubujiza,
    Nikimuomba muweza,
    Amani kutujalia.

    Hapa sasa ndo kikomo,
    Hilo ndilo langu Somo,
    Sitoufunga mdomo,
    Nitazidi kusifia.

  • Pendo

    (Picha kwa hisani ya Adobe Stock)

    Na Abdul Shaban

    (abdoolmtyro@gmail.com)

     

    Ukipenda tafakari lako pendo,
    Unaempambania ana pendo?
    Au unapambana ili upate pendo?

     

    Nakupenda sikatai na wajua,
    Ila bado hunifai my dear,
    Hunipendi sikatai mi najua,
    Ila bado siamini mi nalia.

     

    Nalilia nini zaidi ya pendo?
    Kwako sina meno, mi siumi yani magego,
    Ninakupenda na sijapenda mpango wa kando,
    Hili sio pendo mi naapa hili ni tego.

     

    Hukunipa furaha hata nilipokufurahisha wewe,
    Ukaniacha kwa mataa nikizongwa na mwewe,
    Lako penzi nakataa bora nibaki mwenyewe.

     

    Zile chomoa chomeka humaliza chaji,
    Na hili betri likiisha hakuna wa kulichaji,
    Kutwa utalizungusha ufundi nao kipaji,
    Ghafla nalo lakufa ujione mkosaji.

     

    Kosa si kosa nakataaa,
    Kosa ni kosa hapo sawa,
    Kosa la kunichosha na kunitosa,
    Kosa la kukuposa ni langu na sitabisha.

  • Je, muda wa mshambuliaji wa Manchester United, Christiano Ronaldo, umekwisha Old Trafford?

    (Picha kwa hisani ya News18)

    Na Abdul Shaban

    Manchester United ilitangaza siku ya Alhamisi jioni kwamba Cristiano Ronaldo hatakuwa nao watakaposafiri kwa ndege kwenda Bangkok Ijumaa kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Erik ten Hag akiwa meneja.

     

    Ronaldo ameruhusiwa kusalia Ureno, kwa ruhusa ya United, kushughulikia suala la kifamilia ambalo halijawekwa bayana.

     

    Mchezaji huyo nmwenye umri wa miaka 37 , ikumbukwe, alipoteza mtoto wa kiume mnamo Aprili, wakati mpenzi wake alipojifungua pacha, mmoja tu ndiye alyenusurika.

     

    Hakuna kiasi cha pesa au umaarufu unaoweza kumkinga mtu kutokana na aina hiyo ya kiwewe.

     

    Hata hivyo habari hizo zilijiri siku tano baada ya hamu ya Ronaldo kutaka kuondoka United msimu huu wa kiangazi kuwa hadharani.

     

    Na ingawa hatakuwepo, hiyo itakuwa simulizi ambayo itatawala wakati wote ambapo klabu hiyo itakuwa nchini Thailand, na kisha Australia, ambako watacheza mechi ya Jumanne dhidi ya wapinzani wao wa zamani Liverpool.

     

    Saa moja kabla ya Ronaldo kubainika kwamba hatokuwa katika safari ya kuelekea Thailand , chanzo kimoja kinachoifahamu BBC Sport kilisema kuwa hakukuwa na nafasi ya mchezaji huyo kuwa katika safari hiyo.

     

    Hatua hiyo ilijiri kutokana na imani kwamba Ronaldo lazima alikuwa na mpango wa kuondoka kwasababu , iwapo hataondoka , kile kilichojiri Wikendi kisingefanyika.

     

    Chanzo chengine cha United pia kiliunga mkono hoja hiyo. Wao pia walikubaliana kwamba sakata hiyo itakwisha wakati Ronaldo atakapoondoka katika klabu hiyo alioyowasili kwa mbwembwe za aina yake Agosti iliopita , baada ya kujiunga huku klabu ya Manchester City pia ikiwa na hamu ya kumsajili.

     

    Kwa upande wao Man United inasema kwamba Ronaldo haendi popote , wakidai kwamba ana mwaka mmoja katika kandarasi yake kuondoka kitu kinachomfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika ligi ya premia na kwamba wanatarajia kwamba ataheshimu kandarasi hiyo.

     

    Hata hivyo klabu inapaswa kusema hivyo ili kulinda mali zao. Wanajua kuwa katika soka ni mara chache wachezaji wanashikiliwa na mikataba yao ikiwa wamedhamiria kuondoka, hakika si wachezaji wa hadhi ya juu kama Ronaldo.

     

    Wakati mwingine msimamo huo unaendelea kwa wiki – kama Bayern Munich wanavyofanya sasa na mshambuliaji Robert Lewandowski – lakini kawaida makubaliano hufanywa na mchezaji anapata anachotaka.

     

    Katika hali hii, ajabu ni kwamba haitokani na dhamira ya Ronaldo ya kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu zaidi, na kwamba hali ingeweza kufikia kilele mapema zaidi. Baada ya yote, ilikuwa dhahiri United haingeweza kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa kipindi kirefu kabla ya msimu kufikia kilele chake.

     

    Msisimko wa mechi za kujiandaa kwa msimu mpya

    United wamezoea masuala kama haya kutawala safari zao za mechi za kujiandaa kabla ya msimu mpya.

     

    Miaka mitatu iliyopita, katika ziara yao ya mwisho, kabla ya Covid kuwazuia ghafla, mzozo ulitawaliwa na iwapo Paul Pogba aliyechukizwa angerudi kutoka Marekani kwa wakati ili ndege ielekee Perth. Alifanya hivyo – lakini Romelu Lukaku alidhihirisha hadharani kutoridhika kwake kwa kujielekeza kwenye vikao vya mazoezi ya baiskeli ili apone jeraha ambalo lilipungua mara tu alipoondoka kwenda Inter Milan.

     

    Hiyo ilikuwa ziara ya kwanza ya Ole Gunnar Solskjaer kama meneja wa United. Licha ya kupata uzoefu huo kama mchezaji. Ten Hag anakaribia kugundua ushabiki wa klabu hiyo huko Mashariki mwanzoni – na jina lake kuu halitakuwepo ili kuondoa tahadhari hiyo.

     

    Badala yake, Ten Hag atakapokabiliana na vyombo vya habari – pengine Jumapili – kwa mara ya kwanza tangu lipozinduliwa Old Trafford, atakuwa na maswali mengi ambayo huenda asiwe na majibu – yaani ni lini au ikiwa Ronaldo ataanza kushiriki mazoezi pamoja na wachezaji wenzake.

     

    Je, Ronaldo ndiye suluhu au tatizo?
    Kuna mawazo mawili kuhusu uwepo wa Ronaldo United

    La kwanza ni kwamba alikuwa mmoja wa wachezaji wawili pekee – kipa David de Gea ndiye mwingine – kuibuka kutoka kwa msimu mbaya uliopita bila sifa zao kuingia doa . Alifunga mabao 24, ikiwa ni pamoja na hat-trick mbili, na, bila yeye, United ingekuwa katika hali mbaya zaidi kuliko ile waliyoishia.

    Lakini kuna simulizi nyingine, kwamba Ronaldo alikuwa mmoja ya sababu kuu zilizoifanya klabu kumaliza pale ilipomaliza.

    Inasemekana mara nyingi Ronaldo hapandi juu uwanjani – mkakati uliowekwa na mkufunzi Ralf Rangnick aloitarajia kutekeleza katika klabu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Solskjaer mnamo Novemba. Pia ndio mbinu ilioanzishwa na Ten Hag katika timu yake huko Ajax.

     

    Lakini je, uwepo wa Ronaldo ulikuwa mbaya pia?

    Alitofautiana na Harry Maguire kuhusu unahodha na, kwa kuzingatia hadhi ya Ronaldo, ni rahisi kufikiria angekuwa na maoni ya moja kwa moja kuhusu mambo mengine pia. Aliondoka uwanjani kwa kusuasua mara nyingi baada ya mechi, kwa hivyo anaweza kuwa anasema nini faraghani kutokana na hali mbaya ya jumla Old Trafford?

     

    Ni kweli Ronaldo akienda, United hawana nambari tisa – na hawajamtafuta.

     

    Lakini City wameshinda mataji mfululizo ya Ligi Kuu bila hata moja. Kiuhalisia, matarajio ya United ni ya chini sana na tayari wana idadi ya washambuliaji wa kimataifa wenye kasi ambao, labda, wanaweza kubadilishana. Kuwasili kwa Christian Eriksen kutaongeza ubunifu unaohitajika kwenye kikosi chao. Inatarajiwa kutakuwa na uimara zaidi katika safu ya kiungo hata kama harakati za kumtafuta Frenkie de Jong wa Barcelona zitashindwa kufanikiwa.

     

    Wiki chache zijazo zitakuwa muhimu kwa Hag Kumi.

     

    Anajua Ronaldo atakosekana mwanzoni mwa kipindi chake. Kwa uwezekano wote hatakuwepo kwa safari nzima.

     

    Jukumu la Ten Hag katikia eneo la mashariki na kwingineko ni kuandaa mpango ambao utafaa bila yeye. Msimu wa United unaweza kuutegemea.

  • MTIMA WANGU WAUMA

    (Picha kwa hisani ya Pinterest)

    Na Abdul Shaban

     

    Mwenye hisani ni nani, kwanza ninawauliza,

    Aeleke mtimani, bila hata ya kuwaza,

    Khatari imesheheni, yupo aloniumiza,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Tangazo nilolitoa, makusudio ninayo,

    Sitaki tena madoa, asije kufata nyayo,

    Awe mtuvu kapoa, atulize nilo nayo,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ilio kubwa sababu, sasa nakwenda kusema,

    Moyo aliusulubu, hakunielewa vyema,

    Amri zake wahabu, hakutekeleza hima,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Mapenzi aliyapata, nami yake nilipata,

    Yani alikula bata, vijana wanavyoita,

    Uzuri wa kumemeta, kwa hayo mi sikujuta,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Alinikata kauli, usiku hata mchana,

    Niliposema tuswali, hapo yeye alinuna,

    Niliudhika kwakweli, japo nampenda sana,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Wala sikumdekeza, onyo nikampatia,

    Hapa nitakufukuza, kama ukiendelea,

    Hakutaka kusikiza, nikawa na mbili njia,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Apendezea uzuri, ila nikajawa khofu,

    Kama kuswali khiyari, vipi niwe mkunjufu,

    Nahitaji yenye kheri, toka kwa mola Raufu,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Nikafanya maamuzi, yalopendeza kwa mola,

    Nikaitoa simanzi, na shetwani mwenye hila,

    Tamko lenye majonzi, nakuacha kisa swala,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Gumzo likaenea, familia na mitaani,

    Naye akajiendea, kurudi kwao nyumbani,

    Sitaki kuteketea, kwa ghadhabu za manani,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ukweli nishausema, hayo ndiyo yalojiri,

    Nahitaji mke mwema, kwenye dini yu hodari,

    Nimefika qadetama, nawaageni kwaheri,

    Mtima wangu wauma, nataka wa kunipoza.

     

     

     

  • Sherehe ya Eid-ul-Adha 2022

    (Picha kwa hisani ya Hindustan Times)

    Na Getrude Prosper

    Mwaka huu wa 2022, nchi tofauti tofauti duniani zimesheherekea sikukuu ya Idd kwenye tarehe tofauti. Baadhi ya nchi zimesherehekea siku ya Jumamosi Julai 9 2022 na zingine zimesherehekea siku ya Jumapili Julai 10 2022. Zaidi ya hayo, Waziri wa Usalama wa ndani, Fred Matiang’i ametangaza kuwa Jumatatu, Julai 11 2022 kuwa siku ya mapumziko ya kuadhimisha sikukuu ya Idd-ul-Adha nchini Kenya.

    Idd-ul-Adha ni siku ya kuchinja na huadhimishwa siku ya 10 ya Mwezi wa Dhul-hijjah, mwezi ambao waislamu huenda kuhiji Makka, Saudi Arabia. Sherehe za mwaka huu nchini Kenya zimekua tofauti kidogo kutokana na hali ya uchumi iliyofanya gharama ya maisha kua juu. Baadhi ya wafanyabishara wanadai kua msimu huu wamepata hasara kubwa kwasababu ya kupungua kwa wateja. Kabla ya mabadiliko ya hali ya uchumi, siku za sherehe hua ni siku za wafanyabiashara kuuza zaidi kuliko siku zingine kutokana na misururu ya watu wanokuja sokoni kununua bidhaa mbambali ikiwemo nguo na vyakula.

    Mwaka huu hamna dalili zozote zile za sherehe kwenye baadhi ya maeneo kama awali kutokana na gharama ya maisha kupanda. Vitu vimepanda bei wanunuaji wamepungua.