Category: Jamvi la Kiswahili

  • Tetesi Za Mbappe

    {Picha kwa hisani ya Sky News}

     

    Na Abdul Shaban

     

    Mshambuliaji Kylian Mbappe wiki jana Jumanne aliripotiwa kuwa na kikao maalumu na rais wa Paris Saint-Ger-main, Nasser Al-Khelaifi kujadili hatima yake.  Rais wa PSG Al-Khelaifi alikiri kushtushwa na uamuzi wa mshambuliaji huyo kwamba hawezi kubaki kwenye timu hiyo hadi 2025. Kutokana na hilo, PSG ilimpa Mbappe wiki mbili za kuamua kama anabaki Parc des Princes kwa maana ya kusaini mkataba mpya au la basi auzwe kwenye dirisha hili hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

    Hivyo, Mbappe na Al-Khelaifi walitarajia kukutana jana ana kwa ana ana kwa ajili ya mazungumzo na kuwekana wazi juu ya hatima ya kila upande klabuni hapo. . Kuna ripoti zilidai kwamba Mbappe atakwenda kuambiwa hadi kufikia Julai 31 atatakiwa aweke wazi msimamo wake kama atabaki PSG hadi 2025 au milango ifunguliwe ya kupokea ofa ya kupiga bei mwaka huu.

    Real Madrid bado wanapewa nafasi kubwa ya kunasa saini yake, lakini miamba hiyo ya Bernabeu inaelezwa kwamba haina pesa za kugharimia uhamisho wake baada ya kumtumia mkwanja mrefu kwenye dirisha hili kunasa huduma ya kiungo Jude Bellingham kutoka Borussia Dortmund. . Kutokana na hilo, timu za Ligi Kuu England zinaweza kuingia kwenye mchakato wa kunasa saini yake ikiwamo Manchester United, Arsenal na Liverpool ambazo zote zimeripotiwa kufuatilia kwa karibu mchakato huo.

  • MAKAMU CHANSELA WA CHUO KIKUU CHA DAYSTAR ATEULIWA KAMA MWAKILISHI WA KITAIFA WA BODI YA CHAMA CHA ELIMU YA MAREKEBISHO, MAREKANI.

    [Picha kwa hisani ya Prof. Laban Ayiro Facebook]

     

    Na Ashley Mbashu

     

    Makamu wa chansela, Profesa Laban Ayiro, ateuliwa kuwa mwakilishi wa bodi ya chama cha Elimu ya Marekebisho,  Marekani.

    Chama hiki kinahusu wataalamu wanaofanya kazi kwenye vitengo vya watu wazima na watoto kote nchini. Wao hutoa mafunzo muhimu na mitandao yenye manufaa ili kuwawezesha kuwasilisha maelekezo yenye ufanisi na yenye kuleta mabadiliko kwa wanafunzi wao.

    Shirika hili la kimataifa kiliundwa mnamo mwaka wa elfu moja mia kenda na thelathini. Shirika hili limeweza kuwahudumia watoa nidhamu na mashirika ya elimu ya mabadiliko kote duniani kwa miaka mingi.  Limeweza kutimiza haya yote kupitia uongozi, mwelekeo na huduma wanazotoza. Shirika hili limeibuka la kipekee kwenye utetezi wa kitaalam nchini Marekani.

     

    Kama mwakilishi wa kimataifa wa chama husika, Profesa Laban ana jukumu la kuhakikisha uhusiano mwema kati ya shirika husika na mashirika mengine ya kimataifa,  na taasisi zinazohusika na elimu ya marekebisho na nyanja zisizo za Marekani. Pia, atatakiwa kurahisisha mawasiliano kati ya shirika la kimataifa na washirika wao wa kimataifa.

     

    Profesa Ayiro pia atahitajika kuwakilisha muungano kwenye mikutano ya kimataifa na mingine ambapo pia atatakiwa kushiriki maarifa na kuzungumza kwa niaba ya wanachama wa shirika hilo.

     

    Kuteuliwa huku kwa Profesa Ayiro kwenye nafasi hii kunaonyesha anavyojizatiti kwenye kazi zake na pia uongozi. Ni heshima na fursa kuu kwetu, wanafunzi wa chuo kikuu cha Daystar, kwani tutaweza kujifunza na pia kufuata nyayo zake. Uteuzi huu ni ushahidi wa mafanikio yanayoweza kufanikishwa kupitia bidii za mchwa, kujitolea na cha muhimu, dua.

     

    Sisi kama wanachama wa gazeti la Involvement, tunampa mkono wa pongezi, Makamu chansela, Profesa Laban Ayiro.

     

    Kongole!

  • Pinky Ponky

    [Pcha kwa hisani ya Freepik]
    Na Abdul Shaban.
    Nimefika katikati,kuelekea nyumbani.
    Namuona kaiwesti,nayeye yuko njiani.
    Juu kavalia vesti,chini nguo ya kijani.
    Akauliza bwana J,mbona umekimya sana?
    Mbona umekimya sana,ndio swali alonipa.
    Sikujibu kwamapana,mana nilitaka sepa.
    Njaa ilibana sana,jibu sikuweza mpa.
    Lisilo budi hutendwa,leo tunzi yakujibu.
    Leo tunzi yakujibu, hadhi zetu zilishuka.
    Sasa ikawa wajibu,ndimi zetu kuzisita.
    Walizikosa adabu,tungo zikawa ni vita.
    Tukaachia vijana, wajitao mwendakasi.
    Lugha zao Sheng shengi,wabaranga kiswahili.
    Tungo zao wrong wrongi,nami nikiiga hili.
    Nyimbo zao ping pongi,haohao baradhuli.
    Basi raha ya utashi,kwenye fani ikaenda.
  • WAPI NJIA NITAPATA?

    Na Abdul Shaban

    Ndugu zangu ahlani, wasahlan jamia
    Nawaombea amani, iweni nanyi daima
    Nimenena kwa vinani, taarifa kuwafika
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Mwenzenu nawambieni, limenikuta gharika
    Chonde chonde sikizeni, nipatapo saidika
    Sitanena kwa uwazi, adui atang’amuza
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimo ndani ya bahari, nimezama kwa pupa
    Hali imetahayari, sina hata pa kushika
    Mchana hapapo tuli, usikupo kwachafuka
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nilifanya sana siri, pale nilipompata
    Nikataka msitiri, shida zake kumputa
    Kumbe ndiye baladhuli, wahida hanayo sifa
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Sikufata desturi, nikajivika upapa
    Sikuskiza shauri, uziwi ulinishika
    Nikajivika makini, kumbe sina maarifa
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Baharini si shwari, nimeloa chapachapa
    Maji chumvi kooni, yaniwasha kwa hakika
    Wadudu wa baharini, nawano wanichonyota
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimekuwa maskini, sina hata pakushika
    Kila nikipiga mbizi, maji nayo yanivuta
    Sina cha kujistiri, ngiri nayo yaniliza
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Wapi ndugu majirani, waja wote wanipita
    Mniswamehe jamani, nimejifunza hakika
    Wavuvi na makuhani, kwa pamoya nawaita
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Msiniache jamani, mwenzenu nahangaika
    Nimenena hadharani, mnipe njia kupita
    Nisijepo buriani, nyote mkaumbuka
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimenena bila khini, ili nipate ng’amuka
    Yeye kashika mpini, msijepo kwa pupa
    Chukueni tahadhari, sote aso tuzamisha
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

  • Huzuni Kwa Mama Likizoni

    Na Abdul S. Shaban 

    Mwambie anipigie ni mimi mama yake! Mwambie sina simu ila nimeona picha zake kwenye simu ya kupalaza ya khamisi. Mwambie amenenepa sana ..mwambie nimeona gari lake ni zuri sana ! Ila mwambie mama yake bado naishi kwenye lile banda pamoja na kuku. Mwambie nimeumwa sana ila nikapona bila hata kutumia dawa. Mwambie Mzee Juma bado ananidai pesa zake nilizokopa ili nimlipie ada, amechukua kile kishamba nilichokuwa nakitegemea kufidia deni lake. Mwambie mimi mama yake nimebaki pekee yangu tangu baba yake afariki sina hata wa kunisogezea kuni motoni. Mwambie leo nimetamani sana nyama, zile mboga zilizoota zenyewe upenuni zimenichosha mpaka mdomo umekuwa mchungu. Mwambie wale vijana walitaka wanipige eti mimi mchawi eeh. Mwambie mama yake nimekuwa mzee sana nahesabu siku tu aje hata nishike mikono yake nimuoneshe mipaka ya nyumba yetu! Salio limeisha mwambie mama anampenda sana! Ila huku kijijini nimebaki pekee yangu wenzangu wote wameenda mjini kusherekea kwa watoto wao.

  • MUDA

    {Picha kwa hisani ya HelpGuide.org}

     

    Na Abdul S. Shaban

    Nakumbuka ule muda,
    Niliokuwa napoteza muda,
    Nabaki naumia buda,
    Sikuwahi tunza muda.

    Muda leo unao,
    Muda kesho hunao,
    Muda kama pembejeo,
    Muda upangie vikao.

    Muda usikupe husda,
    Muda gawa wa ibada,
    Muda wapea ka kishada,
    Muda ni chanzo cha mada.

    Muda si kikonkomwe,
    Muda si ardhi ulimwe,
    Muda si boda utumwe,
    Muda ni mali jitume.

    Muda wajada jitihada,
    Muda usiupelekeshe kishada,
    Muda usiuletee kidada,
    Muda si mchepuko kimada.

    Muda wakimbia, haurudi,
    Vuta soksi shikilia, jitahidi,
    Punguza kulia lia, makusudi,
    Usivyovifurahia, usivihimidi.

  • RUKA NAMI

    {Picha kwa hisani ya birdfact}

     

    Na Abdul S. Shaban

    Wewe ni ndege mzuri, zavutia zako mbawa,
    Harufuyo ya uturi, niumwapo ndiyo dawa,
    Nuru yashinda kamari, inawaka maridhawa,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

    Naomba uruke nami, ndiyo ya kwangu maombi,
    Chini kuna tsunami, ina makubwa mawimbi,
    Ukidondoka na mimi, kufa nawe sio dhambi,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

    Ukiweza nami ruka, kiotani kuniacha,
    Napenda vyako vibweka, na kelele kukikucha,
    Naamini tateseka, mpweke ukiniacha
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Turuke wote angani, nipeleke kule juu,
    Nikudekee mwandani, ka bibi na mjukuu,
    Washangae insani, sitaki zao nahau,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Ni radhi kuacha nyumba, kuishi kwenye kiota,
    Walosema ninayumba, wazi wazi watajuta,
    Walochukia uchumba, kilingeni mewakuta,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Sauti ndege wengine, wazipaza kweli kweli,
    Kuna za wale wanene, wenye ukubwa wa mwili,
    Wakatafute pengine, sisikilizi badali,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Tena vyema kunilinda, hilo la kwako jukumu,
    Niliwaze kama kinda, kwa upole na nidhwamu,
    Ninajua wanipenda, moyo meshika hatamu,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

  • MTI ULIOPINDA

    {Picha kwa hisani ya Warren Photographic}

     

    Na Abdul S. Shaban

     

    Hakiwezi kunyooka, kivuli cha mti huu,
    Toto la nyoka ni nyoka, majuto ni mjukuu,
    Maovu ukiyataka, sifanyie mji huu,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kivuli kitafuata, umbile la mti wake,
    Ikiwa kitakupata, mtoto kinyesi chake,
    Hutakiwi kuukata, osha mkono sinuke,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kama hivyo basi ndivyo, twapaswa kuzingatia,
    Mkubwa akiwa ovyo, watoto huiga pia,
    Watafata hivyo hivyo, tabia zilosalia,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kama haujatulia, wapenda kujivinjari,
    Watoto huangalia, mwenendo kuukariri,
    Keshokutwa wasikia, dogo kalewa chakari,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Mavazi wajivalia, vimini ama vinjunga,
    Wana kuwanunulia, barabarani mwatinga,
    Hivyo unavyowalea, vibaya unawajenga,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Hata iwashike dhiki, kunyooka musichoke,
    Kivuli hakinyooki, hufata matawi yake,
    Kwenye hilo tia tiki, mashaka usiyaweke,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Maana nimeiweka, na mwisho ninakomea,
    Kalamu imeandika, usia kuwatolea,
    Munapaswa kuushika, musije kuangamia,
    Kivuli hakinyooki, kama mti ukipinda.

  • TABIA NCHI

    {Picha kwa hisani ya As You Know}

                                                   

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com}

    Tabianchi ni hali ya mabadiliko ya mazingira ya hali ya hewa ikiwemo joto, mvua na pepo. Mabadiliko ya tabianchi yanapojitokeza kunaweza kutokea ongezeko la mawimbi ya joto, mizozo ya kimataifa, mafuriko na ukame unaoathiri viumbe hai.

    Kwa asilimia kubwa, mabadiliko haya yanachangiwa na shughuli za binadamu ikiwemo uchomaji wa makaa na mafuta katika viwanda, vituo vya umeme na kwenye magari.

    Ongezeko la joto linaweza kuleta athari kama vile; viwango vya maji baharini kupanda, bahari kuchemka na kuwa na tindikali zaidi, barafu vya vilele vya milima kuyeyuka na kusababisha mafuriko, kubadilika kwa mikondo ya bahari, ukosefu wa mvua itakayosababisha njaa na uhaba wa maji, ongezeko la halijoto, upepo, tufani na kuenea kwa magonjwa. Zaidi ya hayo, madhara haya yanaweza kusababisha vifo vya watu na viumbe hai kama mimea na wanyama na kuvifanya kutoweka.

    Janga hili la ongezeko la joto linaweza kuepukika ikiwa watu watachukua hatua ya kupanda miti, kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa chafu ya kaboni, kukabiliana na matatizo ya taka yanayojikusanya kwenye mito na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

    Kando na hayo, watu wanaweza pia kujenga nyumba zinazoweza kumiliki mabadiliko ya tabianchi ili kuwa salama. Njia hizi ikiwemo kujenga kwa kuzingatia ukame, viwango vya joto, mafuriko, baridi, vimbunga na upepo mkali.

    Tunatakiwa kuhamisha uwekezaji wetu kutoka kwenye uchumi mchafu kuenda kwenye uchumi msafi unaotumia teknolojia inayowafikia watu wote katika nchi zote.

  •   BIASHARA YA OMBAOMBA

    {Picha kwa hisani ya Mwananchi}

     

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com} 

    Tumekua tukiona watu ikiwemo watoto na wazee walemavu barabarani wakiombaomba ili waweze kujikimu kimaisha. Ila cha kushangaza ni kwamba wengi wao wapo kibiashara, na sio tu biashara ya kawaida ila ni ile ya kutumikishwa.

    Baadhi ya watu hawa wanageuza kuwa mtaji, na nyuma yao ni watu wenye uwezo wanaowatumia ili kunufaika na kufaidi hizo hela au msaada unaotolewa kwa watu hawa. Kisichoaminika ni kua pesa hizo hupitia hesabu ya hali ya juu kama tu mapato mengine. Walemavu wengi hulazimishwa kutimiza matakwa ya waajiri wao ingawa hawaipendi kazi hiyo, kwani “Lisilo budi hutendwa.” Wengine wao wanahadaiwa kua wanatajirika katika biashara hio lakini mwishowe wanateswa, kunyanyaswa na kulipwa kiasi kidogo kisichowatosha.

    Changamoto inatokea pale mtu anapotaka kuwasaidia watu hawa wasiojiweza, anashindwa kujua nia ya kweli ya watu hao wanaohitaji msaada, kumbe wapo hapo kwa kulazimishwa.

    Watoto walemavu pia wanalazimishwa kuomba mitaani na wasipoleta pesa hua wanapigwa. Familia nyingi zinadanganywa kuwatoa watoto wao na kuenda kufanyishwa biashara ya kikatili na haramu. Watoto hawa wanasafirishwa na kuletwa kuja kutumikishwa mbali na wazazi wao na kulamishwa kukatika mawasiliano na wao.

    Kwa watoto wanaotumikishwa, imegundulika kua chanzo ni malezi. Wazazi au walezi wanadanganywa watoe watoto walemavu na kupewa ahadi kua watapewa misaada ya kifedha kama malipo yao ilhali watoto hao wanaenda kuteswa. Wazazi na walezi hawa wanatakiwa kuzingatia malezi ya watoto wao walemavu na kuhakikisha hawakati  tamaa kwa watoto hao na badala yake kuwalinda ili kuepukana na mazingira hatarishi. Jamii pia inatakiwa kuhakikisha kwamba watoto hawa walemavu wanalindwa ili wawe raia wema na sio mzigo kwa Taifa. Sio watoto tu, hata wazee walemavu wanahitaji ulinzi kwa sababu wanyanyasaji hawa wananufaika wakijua watu hawa wenye ulemavu hawajiwezi na wengine wametelekezwa.

    Hata hivyo, mbali na hawa wasiojiweza kutumikishwa, kuna walemavu, wanaofanya ajira hii kwa hiari kutokana na hali yao ya maisha kua ngumu, na hio ndio njia pekee itakayowawezesha kuishi na kutunza familia zao kwa wale wenye watoto. Wamama wenye watoto walemmavu au wamama mlemavu wenye watoto na wameachwa na waume zao kutokana na hali yao, huteseka sana. Walemavu hawa wanakubali kutumiwa kama vitega uchumu ingawa ni kwa mateso, kwani kwao “heri nusu shari kuliko shari kamili”.

    Hali nyingine ni ya ombaomba tapeli, ambayo pia ni biashara inayofanywa na baadhi ya watu wanaojifanya walemavu wakiombaomba ilhali si walemavu bali ni matapeli. Watu hawa wameamua kuanza biashara hii kwani wanaamini kuwa watu huwasaidia au kuwapa fedha watu wenye ulemavu tu. Mwisho wa siku, utawaona watu hawa wakielekea nyumbani bila ulemavu wowote, baada ya kuvuna ambapo hawakupanda.

    Watu hawa utawaona wakitambaa barabarani wakiwa wamevaa mavazi yaliyochakaa kabisa ili watu wengine waamini kuwa hawajiwezi. Kuna baadhi yao pia hukodisha watoto wao au wa ndugu na kuwatumia kama kitega uchumu ili tu wahurumiwe na kuchangiwa pesa. Wengi wao hutumia usafiri wa bodaboda ili wasionekane au kujulikana na watu.

    Biashara hizi za ombomba ni kinyume na sheria kwani inawazuia watu wenye ulemavu kutopata msaada kwasababu ya uoga uliojawa watu ya kuwa wanatapeliwa. Wapita njia wengi na hata waendesha magari wamepunguza kiasi cha kuwasaidia ombaomba barabarani kwa sababu wengi wao hawana ulemavu na hawaaminiki.

    Serikali inatakiwa kuwasaidia walemavu hawa na kuwashika hao matapeli  wanaojifanya.