Category: Mashairi

  • MGENI KIPOFU

    (Picha kwa hisani ya MuseumNext)

     

    Na Abdul S. Shaban

     

    Tazama bila ya hofu, hapo ndipo utaona,
    Alosema muongofu, alitazama kwa kina,
    Pasinapo hitilafu, mimi naye naungana,
    Kuwa mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Mgeni huwa kipofu, hata kama anaona,
    Vitu vyenye upotofu, hasemi atauchuna,
    Huwa anaudhohofu, mjuvi kuonekana,
    Kweli mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Hata aone mnofu, nayo pilau imefana
    Huku njaa takatifu, mgeni imembana,
    Kusema ni ualifu, japo aona bayana,
    Haki mgeni kipofu, hata kama anaona.

    Mwisho ninawaarifu, wa juzi, leo na jana,
    Muone na msadifu, wala hamtabishana,
    Zaidi utamsifu, mjumbe wake Rabbana,
    Haki mgeni kipofu, hata kama anaona.

  • Penzi Halijaribiwi, Utanaswa Unasike.

    (Picha kwa hisani ya The Economic Times)

    Na Abdul Shaban

     

    Mapenzi ya siku hizi, ni ya nipe ndo nikupe,

    Tena ya tele mapozi, kadhalika na mapepe,

    Sipo jali tawa chizi, ujipake na matope,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Penzi halina mjuzi,  nina kwambia peupe,

    panga yako mamuzi, mabaya uje utupe,

    ya sikutoke machozi, yakalovya zako hope,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Mapenzi toka awali, yaliwashinda wa kale,

    Usijione mkali, utarudi na tandale,

    Samsoni nguvu kali, alinaswa palepale,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Ukijifanya bahili, kutosikia wavyele,

    Utashikika pahali, upige zako kelele,

    Kusifiwa ni muhali, huwezi kusonga mbele,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Kujipiga na kifua, eti wewe umakini,

    Utakuja kujutia, ushindwe na kibaini,

    Utalia na dunia, uhame nako nyumbani,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

     

     

    Mwisho nikimalizia, kwa huu wangu waraka,

    Polepole kuanzia, sikuwa nayo haraka,

    Nadhani mumesikia, madada na kina kaka,

    Penzi halijaribiwi, utanaswa unasike.

  • Nakusifia

    (Picha kwa hisani ya WBUR)

    Na Abdul Shaban

    Mke ninakusifia,
    Mzuri umetulia,
    Na wala sitojutia,
    Kifua nakitanua.

    Nakupongeza kwa hili,
    Nyumbani nikiwasili,
    Moyo wangu huwa tuli,
    Hali unanijulia.

    Nilipanga mikakakati,
    Masijidi nikaketi,
    Dua pia na swalati,
    Nikamuomba jalia.

    Nikataraji mazuri,
    Mwenye dini ndo mzuri,
    Mola akanitabiri,
    Wewe ndo ukanijia.

    Sitara unatimiza,
    Mazuri wanihimiza,
    Kikosea wanijuza,
    Toba nije kutubia.

    Wanihimiza kwakweli,
    Nichume yalo halali,
    Adhabu zake Jalali,
    Kwangu unanihofia.

    Hongera we mke wangu,
    Wanilelea wanangu,
    Malezi yaso machungu,
    Mola wao kumjua.

    Naomba kwake manani,
    Tusitengane ndoani,
    Wenye shari maishani,
    Wacheze pata potea.

    Zimekujaa swifati,
    Mahabuba habibati,
    Nitazimaliza beti,
    Sifa hazitoishia.

    Utenzi naumaliza,
    Machozi nabubujiza,
    Nikimuomba muweza,
    Amani kutujalia.

    Hapa sasa ndo kikomo,
    Hilo ndilo langu Somo,
    Sitoufunga mdomo,
    Nitazidi kusifia.

  • Pendo

    (Picha kwa hisani ya Adobe Stock)

    Na Abdul Shaban

    (abdoolmtyro@gmail.com)

     

    Ukipenda tafakari lako pendo,
    Unaempambania ana pendo?
    Au unapambana ili upate pendo?

     

    Nakupenda sikatai na wajua,
    Ila bado hunifai my dear,
    Hunipendi sikatai mi najua,
    Ila bado siamini mi nalia.

     

    Nalilia nini zaidi ya pendo?
    Kwako sina meno, mi siumi yani magego,
    Ninakupenda na sijapenda mpango wa kando,
    Hili sio pendo mi naapa hili ni tego.

     

    Hukunipa furaha hata nilipokufurahisha wewe,
    Ukaniacha kwa mataa nikizongwa na mwewe,
    Lako penzi nakataa bora nibaki mwenyewe.

     

    Zile chomoa chomeka humaliza chaji,
    Na hili betri likiisha hakuna wa kulichaji,
    Kutwa utalizungusha ufundi nao kipaji,
    Ghafla nalo lakufa ujione mkosaji.

     

    Kosa si kosa nakataaa,
    Kosa ni kosa hapo sawa,
    Kosa la kunichosha na kunitosa,
    Kosa la kukuposa ni langu na sitabisha.

  • MTIMA WANGU WAUMA

    (Picha kwa hisani ya Pinterest)

    Na Abdul Shaban

     

    Mwenye hisani ni nani, kwanza ninawauliza,

    Aeleke mtimani, bila hata ya kuwaza,

    Khatari imesheheni, yupo aloniumiza,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Tangazo nilolitoa, makusudio ninayo,

    Sitaki tena madoa, asije kufata nyayo,

    Awe mtuvu kapoa, atulize nilo nayo,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ilio kubwa sababu, sasa nakwenda kusema,

    Moyo aliusulubu, hakunielewa vyema,

    Amri zake wahabu, hakutekeleza hima,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Mapenzi aliyapata, nami yake nilipata,

    Yani alikula bata, vijana wanavyoita,

    Uzuri wa kumemeta, kwa hayo mi sikujuta,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Alinikata kauli, usiku hata mchana,

    Niliposema tuswali, hapo yeye alinuna,

    Niliudhika kwakweli, japo nampenda sana,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Wala sikumdekeza, onyo nikampatia,

    Hapa nitakufukuza, kama ukiendelea,

    Hakutaka kusikiza, nikawa na mbili njia,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Apendezea uzuri, ila nikajawa khofu,

    Kama kuswali khiyari, vipi niwe mkunjufu,

    Nahitaji yenye kheri, toka kwa mola Raufu,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Nikafanya maamuzi, yalopendeza kwa mola,

    Nikaitoa simanzi, na shetwani mwenye hila,

    Tamko lenye majonzi, nakuacha kisa swala,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Gumzo likaenea, familia na mitaani,

    Naye akajiendea, kurudi kwao nyumbani,

    Sitaki kuteketea, kwa ghadhabu za manani,

    Mtima wangu wauma, nani aje kunipoza.

     

    Ukweli nishausema, hayo ndiyo yalojiri,

    Nahitaji mke mwema, kwenye dini yu hodari,

    Nimefika qadetama, nawaageni kwaheri,

    Mtima wangu wauma, nataka wa kunipoza.

     

     

     

  • SAFARI YA UMAUTI

    Na Abdul Shaban

     

    Maradhi yamenisibu, hadi leo naugua,

    Sasa naona aibu, afya imenipotea,

    Naomba kwake Wahabu, kwa rehema za jalia,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Naumwa nakondeana, dawa haziwezi tibu,

    Na kula siwezi tena, ameshasema tabibu,

    Ndugu wanawaza sana, waketi nami karibu,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Nikitizama kushoto, kisha narudi kulia,

    Baba lamtoka jasho, mama naye analia,

    Kauli ni changamoto, kinywani imepotea,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Muda unakaribia, kwa dalili nilo nazo,

    Mauti yanifikia, hilo halina vikwazo,

    Naona amenijia, asohitaji mawazo,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Sakaratil mauti, nilikuwa nasikia,

    Kiu ndo hakikauki, hata maji ya dunia,

    Makosa hayajifuti, madogo nilodhania,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Siwezi tena kutubu, kwa makosa nilofanya,

    Nimekuwa kama bubu, kwa uzito wake kinywa,

    Mauti yaniadhibu, na roho ninapokonywa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Taarifa zatolewa, wengi wanahuzunika,

    *”Kweli tumeondokewa,na mpendwa bila shaka”*

    Kitandani natolewa, uchafu unanitoka,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Ndugu zangu na rafiki, wote wanalialia,

    Na wengine wameketi, eti wananiombea,

    Du’a zao hazifiki, natamani waambia,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Wanatafutwa wajuzi, tayari kuandaliwa,

    Wanikosha kwa simanzi, na marashi kufushiwa,

    Tayari mekwisha kazi, nje sasa natolewa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Simanzi imegubika, baada ya kutolewa,

    Madeni kutangazika, nadai na kudaiwa,

    Swafu witri zimefika, ninaanza kuswaliwa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Mbiombio napelekwa, kaburini kufukiwa,

    Tayari nimeshazikwa, huku watu wahusiwa,

    Mimi nimeshachafukwa, kwa maswali ninopewa,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

     

    Tubuni tubuni jama, kaburi lina vituko,

    Hapa mbavu zimebanwa, natamani rudi huko,

    Walau kwa moja jema, muda tena ndo haupo,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Nashauri walimwengu, tupunguzeni machafu,

    Na tuweni wachamungu, tusimuudhi Raufu,

    Pepo pahala pa mungu, hawapelekwi wachafu,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

    Wanadamu jihadhari, tusije kuangamia,

    Tusifanye ya khatari, mola atuangalia,

    Tuiandae safari, mema tukisubiria,

    Kifo ni njia ya haki, safari yake lazima.

     

  • ENYI VIJANA

    (Picha kwa hisani ya Owlcation.com)

    Na Abdul Shaban

     

    Tulisifu na kulitukuza jina lake siku zote

    Kwa maana anatupenda sisi sote

    Uwepo wake umedhihirika kote duniani

    Siku zote nuru za nguvu zake huonekana hata gizani

    Wakati wa furaha na majonzi na dhiki

    Yeye ndiye dereva wa maisha yetu

     

    Enyi vijana, njooni nyote kwake Jalali

    Yeye ndiye mweza wa yote na aliye halali

    Tujiepushe na yale yanayomchukiza

    Tuwe tayari tuitwapo kusikiza

    Yake masharti kuyafuatilia daima

    Ili maisha yetu yaweze kusimama hima

     

    Enyi vijana, tuwe chombo cha kueneza amani

    Ili mioyo ya wazee na kote duniani iwe na furaha isiyo na kifani

    Tujiepushe na yale yanayoeneza chuki

    Bali tulitengeneza chakula cha ujirani wema kama asali kwa nyuki

    Tupige magoti tusali kwa Mola tukiomba dua

    Kuwa kila siku tuweze kuvutia kama ua

     

    Enyi vijana, yakini tukumbuke tulikotoka

    Tubadilishe yetu mienendo ili tupate kuokoka

    Tusiwe na mioyo mizito ilijaa takataka

    Bali tuombe msamaha kwake Mola mkono wake wa kulia tutakaa

    Tuweze kusimama imara katika imani yetu

    Tukijua ya kwamba mola hujibu maombi yetu

    Na yule amwaminiye hawezi kumwacha ateseke kamwe.

  • KITU KIZITO

    (Picha kwa hisani ya Dreamstime.com)

    {Na Abdul Shaban}

     

    Nakumbuka siku hiyo, niliketi kitandani,

    Alikuja mbiyombiyo, akalala kifuani,

    Akiwa mwenye kiliyo, kama yuko msibani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kabla kumuuliza, tatizo ni kitu gani,

    Ambacho kinamliza, akatoka furahani,

    Akanambia sikiza, “ewe wangu wa hubani”

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Na mimi sikupuuza, kulifanyia utani,

    Sauti nikapunguza, ya redio pale ndani,

    Akaanza kunijuza, ili kunitoa dhani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kwa sauti ya kuimba, kama chiriku mbugani,

    Ndipo akaanza amba, kimtiacho shidani,

    Kuwa eti! Ana mimba, ni yangu si ya fulani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Sikusubiri apoe, ama afike mwishoni,

    Ikabidi niyatoe, niliyonayo moyoni,

    Nikaanza na mayoe, yalonijaa pomoni,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    “Nyonda wangu taratibu, sikiza yangu maoni,

    Japo jambo la aibu, mimba isiyo ndoani,

    Kulea ninawajibu, usiwe mwenye sononi”

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Kwangu ikawa aula, sote tukiwa rahani,

    Nikazidi saka hela, viwe havikosekani,

    Vizurizuri vyakula, matunda pale nyumbani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Ikakatika miezi, kwa rehema za Manani,

    Nikiyatoa malezi, mzuri yenye thamani,

    Akabariki Menyezi, kujifungua mwendani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Huku nikiwa na hamu, nikawasili gangoni,

    Mtoto nimfahamu, aliyetoka tumboni,

    Sikuamini dawamu, nilichoona machooni,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Ayi! Nilipata tabu, sijawahi maishaini,

    Nikaiona ajabu, mbaya isiyo mfani,

    Ati! Napewa mwarabu, na mie hatufanani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.

     

    Tama naachia nibu, kuongeza sitamani,

    Nyonda hana la kujibu, anaomba samahani,

    Kwa haya yalonisibu, siwezi kutamakani,

    Hakika kitu kizito, kimenipiga kichwani.