Category: Mashairi

  • TUNACHORA KESHO HAPA

    Na Chelangat Caren,

     

    Tunasimama hapa, kati ya vitabu na ndoto,

    Miguu yetu ardhini, macho yetu juu angani,

    Kila ukumbi ni uwanja wa vita na ushindi,

    Kila usiku mweupe ni shahidi wa jitihada zetu.

     

    Sisi ni wimbo wa matumaini yasiyochoka,

    Tukiimba kwa sauti ya HELB, na majibizano ya CAT,

    Tukipambana na usingizi ili tuibe dakika za maarifa,

    Kwa sababu tunajua: maarifa ndiyo ufunguo wa milango iliyofungwa.

     

    Hapa chuoni hatujifunzi hesabu peke yake,

    Tunajifunza uvumilivu wakati rafiki anapoondoka ghafla,

    Tunajifunza ujasiri wakati wazo letu linapotukanwa darasani,

    Na tunajifunza upendo wakati mgonjwa anapopata jani la sala kutoka kwa mgeni.

     

    Usidhani machozi ya usiku wa mtihani ni udhaifu,

    Hayo ni mchanga unaochonga jiwe liitwalo “mimi mpya.”

    Siku moja tutasimulia hadithi hizi kwa kicheko,

    Na kusema: “Tulikuwa hapo, tulichoka, lakini hatukuvunjika.”

     

    Kwa hivyo mwanafunzi mwenzangu, shika kalamu yako,

    Chora ndoto yako kwenye ukurasa wa maisha haya.

    Kwa sababu kesho tunayoitafuta haiko mbali,

    Inaanzia hapa—katika sakafu hii ya chuo, katika moyo huu usiokata tamaa.

     

    Na siku itakapoingia historia, wataniuliza:

    “Ulikuwa wapi wakati ulimwengu ulipobadilika?”

    Nitasimama mnyoofu niseme:

    “Nilikuwapo. Nilikuwapo nikijenga kesho yangu hapa chuoni.”

  • SAUTI YA KESHO

    Na Chelangat Caren,

    IEBC

     

    Kujenga kesho ni sasa,

    Sauti yako ni nguvu, usiache,

    Wahenga walisema, “Mtu ni watu,”

    Siasa si uchafu, ni hatua.

     

    Kura yako ni sauti, itamke,

    Chagua viongozi, wasio na wake,

    Wananchi wa kwanza, si familia,

    Umoja na maendeleo, ni njia.

     

    Usikubali kupuuzwa, usiogope,

    Siasa ni ajira, ni maisha,

    Jenga taifa lako, kwa mikono yako,

    Kenya mpya, ni wewe na mimi, sote.

     

    Siku ya kura, ni siku ya haki,

    Usikose, fanya sauti yako isikike,

    Kiongozi wa kesho, ni wewe,

    Youth, amka, Kenya inakuita  .

     

    Simama imara, kama mlima wa Kenya,

    Sauti yako ni silaha, itumie,

    Changamkia fursa, ya uongozi,

    Kenya inakuita, usikawie.

     

    Maamuzi ya leo, yanabuni kesho,

    Usikubali rushwa, au propaganda,

    Chagua mustakabali, wenye maendeleo,

    Kenya mpya, ni wewe na mimi, sote.

  • Tumepanda Mbegu

    Na Chelangat Caren chelangatcaren756@gmail.com,

    Vecteezy

     

    Tumepanda mbegu, za elimu ndani ya mioyo,

    Tukiitumaini kesho, iliyo bora zaidi,

    Nuru ya maarifa, inatuongoza,

    Katika njia ya mafanikio, bila kuzuilwa.

     

    Walimu ni taa, zinazotuongoza,

    Kuelekea ndoto zetu, bila hofu wala khofu,

    Tunasoma kwa bidii, tukiwa na shauku,

    Ili tulete maendeleo, kwa taifa letu.

     

    Kila siku ni fursa, ya kujifunza na kukua,

    Tukiwa na marafiki, tunaunda kumbukumbu.

    Shule ni bustani, ya maarifa na ndoto,

    Ambapo tunajifunza, na kufanikiwa kwa pamoja.

     

    Tumepanda mbegu, za matumaini na ndoto,

    Na tunazisubiri, kwa hamasa na furaha.

    Kesho itakuwa, ya wale wanaojitahidi,

    Na ndoto zao zitakuwa, ukweli utakaopita.

     

    Tumepanda mbegu, za elimu na ndoto,

    Na tutazichuma, kwa bidii na juhudi zetu.

  • Sikitiko la moyo

    Na Mariita Joshua 

    Langu sikitiko ni haja ya moyo,

    Moyo wenye kuvunjika na kuvunda,

    Makovu yangalipo kama alama ya utambulisho.

    Nisijafa ili nililiwe ila vikao naviona jinamizini,

    Furaha imenikoma ili wimbi la kiza litawale,

    Nani wakunipa mapendo ili mtima udunde?

    Mbona raha inikauke wakati chemichemi inabubujika?

    Nguvu sinazo, ni lelemama jina langu,

    Hawahitaji kwenda vichekeshoni,

    Mwenyewe ningalipo kitimbwi,

    Pembeni nimevikwa kirauni, mashaka mie!

    Kama matambara nimeraruka,

    Afadhali nipige deki matapishi yalozagaa sakafuni,

    Nikanyagwe na wenyeji kwa wageni,

    Nitumbukizwe majini niloe nifinyangwe.

    Wakila vitamu nilambishwe munyu,

    Niwe na ndia ndefu ya kuibusu asubuhi ifatayo,

    Nikorome kochini matumbo yakikohoa,

    Shadidi inikumbate nikauke kama aiskrimu.

    Niwe Kinyago kokote,

    Wa kuonwa niwe ila kusikiwa aa!

    Ninyate ili guu lisiporomoshe mwendo

    Nijambe ila lisinuke, niwe kimyaaa!

  • NYAMA NI ILE ILE

    {Picha kwa hisani ya Organic Authority}

     

    Na Abdul Shaban

     

    Mabucha utabadili, nyama ni ile ile
    Wa kizungu na swahili, uitakayo uile
    Kwa chumvi na pilipili, hata uunge tungule
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Nyama zote mabuchani, zatoka machinjioni
    Hizo ndo zenye idhini, zipikwe kwako nyumbani
    Umbile lisikukhini, minofu ilosheheni
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Uzuri wa kula wali, usiule kwa tembele
    Hata ikiwa ugali, chuzi si kipau mbele
    Njaa ikikukong’oli, siyo chochote ukile
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Iwe nyama ya mnofu, ama ile ya mfupa
    Usikukhini upofu, kutotaka toka kapa
    Kuparamia nyamafu, dhana kwamba ndiyo supa
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Nyama ilofungashoni, hiyo ndiyo yakufaa
    Uile kama pudini, wima ima ukikaa
    Alokuridhi #Manani, halali kwako asaa
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Uzuri wa kula nyama, ukosheke fuadini
    Sihadaike mtima, viso kwako mkononi
    Kutwa ukazisakama, eti uwe furahani
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

    Fumbo hili ni jepesi, ulifumbue hadhira
    Sijafanya udamisi, ni insafu nimechora
    Wala si utusitusi, ila yangu tabasura
    Mabucha usibadili, nyama ni ile ile

  • Pinky Ponky

    [Pcha kwa hisani ya Freepik]
    Na Abdul Shaban.
    Nimefika katikati,kuelekea nyumbani.
    Namuona kaiwesti,nayeye yuko njiani.
    Juu kavalia vesti,chini nguo ya kijani.
    Akauliza bwana J,mbona umekimya sana?
    Mbona umekimya sana,ndio swali alonipa.
    Sikujibu kwamapana,mana nilitaka sepa.
    Njaa ilibana sana,jibu sikuweza mpa.
    Lisilo budi hutendwa,leo tunzi yakujibu.
    Leo tunzi yakujibu, hadhi zetu zilishuka.
    Sasa ikawa wajibu,ndimi zetu kuzisita.
    Walizikosa adabu,tungo zikawa ni vita.
    Tukaachia vijana, wajitao mwendakasi.
    Lugha zao Sheng shengi,wabaranga kiswahili.
    Tungo zao wrong wrongi,nami nikiiga hili.
    Nyimbo zao ping pongi,haohao baradhuli.
    Basi raha ya utashi,kwenye fani ikaenda.
  • WAPI NJIA NITAPATA?

    Na Abdul Shaban

    Ndugu zangu ahlani, wasahlan jamia
    Nawaombea amani, iweni nanyi daima
    Nimenena kwa vinani, taarifa kuwafika
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Mwenzenu nawambieni, limenikuta gharika
    Chonde chonde sikizeni, nipatapo saidika
    Sitanena kwa uwazi, adui atang’amuza
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimo ndani ya bahari, nimezama kwa pupa
    Hali imetahayari, sina hata pa kushika
    Mchana hapapo tuli, usikupo kwachafuka
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nilifanya sana siri, pale nilipompata
    Nikataka msitiri, shida zake kumputa
    Kumbe ndiye baladhuli, wahida hanayo sifa
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Sikufata desturi, nikajivika upapa
    Sikuskiza shauri, uziwi ulinishika
    Nikajivika makini, kumbe sina maarifa
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Baharini si shwari, nimeloa chapachapa
    Maji chumvi kooni, yaniwasha kwa hakika
    Wadudu wa baharini, nawano wanichonyota
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimekuwa maskini, sina hata pakushika
    Kila nikipiga mbizi, maji nayo yanivuta
    Sina cha kujistiri, ngiri nayo yaniliza
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Wapi ndugu majirani, waja wote wanipita
    Mniswamehe jamani, nimejifunza hakika
    Wavuvi na makuhani, kwa pamoya nawaita
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Msiniache jamani, mwenzenu nahangaika
    Nimenena hadharani, mnipe njia kupita
    Nisijepo buriani, nyote mkaumbuka
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

    Nimenena bila khini, ili nipate ng’amuka
    Yeye kashika mpini, msijepo kwa pupa
    Chukueni tahadhari, sote aso tuzamisha
    Nawauliza jamani, wapi njia nitapata?

  • MUDA

    {Picha kwa hisani ya HelpGuide.org}

     

    Na Abdul S. Shaban

    Nakumbuka ule muda,
    Niliokuwa napoteza muda,
    Nabaki naumia buda,
    Sikuwahi tunza muda.

    Muda leo unao,
    Muda kesho hunao,
    Muda kama pembejeo,
    Muda upangie vikao.

    Muda usikupe husda,
    Muda gawa wa ibada,
    Muda wapea ka kishada,
    Muda ni chanzo cha mada.

    Muda si kikonkomwe,
    Muda si ardhi ulimwe,
    Muda si boda utumwe,
    Muda ni mali jitume.

    Muda wajada jitihada,
    Muda usiupelekeshe kishada,
    Muda usiuletee kidada,
    Muda si mchepuko kimada.

    Muda wakimbia, haurudi,
    Vuta soksi shikilia, jitahidi,
    Punguza kulia lia, makusudi,
    Usivyovifurahia, usivihimidi.

  • RUKA NAMI

    {Picha kwa hisani ya birdfact}

     

    Na Abdul S. Shaban

    Wewe ni ndege mzuri, zavutia zako mbawa,
    Harufuyo ya uturi, niumwapo ndiyo dawa,
    Nuru yashinda kamari, inawaka maridhawa,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

    Naomba uruke nami, ndiyo ya kwangu maombi,
    Chini kuna tsunami, ina makubwa mawimbi,
    Ukidondoka na mimi, kufa nawe sio dhambi,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami.

    Ukiweza nami ruka, kiotani kuniacha,
    Napenda vyako vibweka, na kelele kukikucha,
    Naamini tateseka, mpweke ukiniacha
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Turuke wote angani, nipeleke kule juu,
    Nikudekee mwandani, ka bibi na mjukuu,
    Washangae insani, sitaki zao nahau,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Ni radhi kuacha nyumba, kuishi kwenye kiota,
    Walosema ninayumba, wazi wazi watajuta,
    Walochukia uchumba, kilingeni mewakuta,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Sauti ndege wengine, wazipaza kweli kweli,
    Kuna za wale wanene, wenye ukubwa wa mwili,
    Wakatafute pengine, sisikilizi badali,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

    Tena vyema kunilinda, hilo la kwako jukumu,
    Niliwaze kama kinda, kwa upole na nidhwamu,
    Ninajua wanipenda, moyo meshika hatamu,
    Ewe ndege ulo mwema, naomba uruke nami

  • MTI ULIOPINDA

    {Picha kwa hisani ya Warren Photographic}

     

    Na Abdul S. Shaban

     

    Hakiwezi kunyooka, kivuli cha mti huu,
    Toto la nyoka ni nyoka, majuto ni mjukuu,
    Maovu ukiyataka, sifanyie mji huu,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kivuli kitafuata, umbile la mti wake,
    Ikiwa kitakupata, mtoto kinyesi chake,
    Hutakiwi kuukata, osha mkono sinuke,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kama hivyo basi ndivyo, twapaswa kuzingatia,
    Mkubwa akiwa ovyo, watoto huiga pia,
    Watafata hivyo hivyo, tabia zilosalia,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Kama haujatulia, wapenda kujivinjari,
    Watoto huangalia, mwenendo kuukariri,
    Keshokutwa wasikia, dogo kalewa chakari,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Mavazi wajivalia, vimini ama vinjunga,
    Wana kuwanunulia, barabarani mwatinga,
    Hivyo unavyowalea, vibaya unawajenga,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Hata iwashike dhiki, kunyooka musichoke,
    Kivuli hakinyooki, hufata matawi yake,
    Kwenye hilo tia tiki, mashaka usiyaweke,
    Kama mti ukipinda, kivuli hakinyooki.

    Maana nimeiweka, na mwisho ninakomea,
    Kalamu imeandika, usia kuwatolea,
    Munapaswa kuushika, musije kuangamia,
    Kivuli hakinyooki, kama mti ukipinda.