Category: Habari

  • KAYOLE INAOMBOLEZA

    Na Chelangat Caren,

    Jioni ya Mei 18, 2026, maneno hayo yalirudi kwa wengi wa Nairobi kama mshale. Siku hiyo, sauti ya Rachael Wandeto ilinyamaza milele. Mwanamuziki wa injili, mama, dada, na sauti iliyokuwa ikisikika kanisani na mitandaoni, alifariki katika shambulio la moto linaloshukiwa kuwa la kisiasa;alikua na miaka 31 tu.

    Rachael hakuzaliwa maarufu. Alikulia Kayole, akipanda daladala asubuhi na mapema kwenda mazoezi ya kwaya Buru Buru. Marafiki zake wanasema alikuwa wa kwanza kufika na wa mwisho kuondoka. “Kama hukuimba kwa moyo, usiimbe kabisa,” alikuwa akiwaambia watoto wa Sunday School walipomzunguka baada ya ibada.

    Wimbo wake wa kwanza, “Nitashinda”, ulivuma mwaka 2023. Sio kwa sababu ulikuwa na beat nzito, bali kwa sababu ulikuwa na ukweli. Rachael aliimba kuhusu kufeli, kupona, na kuamka tena. Vijana wengi waliuona kama wimbo wao wa maisha.

    YouTube yake ilifikia watazamaji 200,000 kwa muda wa miezi sita. Alikuwa anakaribia kutoa album yake ya pili. Ilitokea Kayole, nyumbani kwake. Majirani wanasema waliona watu wawili wakishuka kwenye pikipiki muda mfupi kabla ya moto kuwaka. Ndani, Rachael alikuwa peke yake. Mumewe alikuwa kazini Mombasa, watoto wawili kwa shangazi.

    Moto ulizima kabla ya kufika vyumba vya jirani, lakini chumba cha Rachael kiliteketea. Polisi wanasema uchunguzi unaendelea, lakini tayari kuna uvumi kuwa ilikuwa kulipiza kisasi kisiasa. Rachael hivi karibuni alikuwa amechapisha wimbo unaokosoa unyanyasaji wa kisiasa dhidi ya vijana.

    “Kama ni siasa ilimuuwa, basi tumepoteza zaidi ya mwanamuziki,” aliandika mmoja wa mashabiki zake X. “Tumepoteza dhamiri. “Habari ya kifo chake ilisambaa haraka. Kanisa la PCEA Kayole lilijaa siku iliyofuatia. Vijana walibeba mabango yakiandika “Rachael, Uliimba Kwa Sisi”

    Mike Sonko alifika na maua meupe. Eric Omondi, ambaye siku moja kabla alikuwa mtaani na jerricans tupu, alisimama nje ya nyumba yake na kusema, “Hii si siasa tena. Hii ni maisha ya mtu.”

    Mitandaoni, hashtag #JusticeForRachael ilipanda hadi nafasi ya pili nchini. Wasanii kama Mercy Masika na Guardian Angel walipakia video wakilia na kuimba mistari yake.Lakini kati ya machozi yote, kitu kimoja kilirudiwa: Rachael alikuwa wa watu wa kawaida. Hakuwahi kusahau Kayole. Alikuwa anafadhili masomo ya watoto watatu wa yatima. Alikuwa ananunua unga kwa wajane wa kanisani kila mwisho wa mwezi.

    Mazishi yatafanyika Jumamosi nyumbani kwao Kisii. Lakini tayari wengi wanasema Rachael hatazikwa kweli. Kila wakati kijana anapopata nguvu ya kusimama baada ya kuanguka, anaimba “Nitashinda”. Kila wakati mama anaposhindwa kulipia nauli lakini bado anaamini kesho itakuwa njema, anasikia sauti ya Rachael.

    Siasa inaweza kuchoma nyumba. Risasi inaweza kunyamaza mdomo. Lakini wimbo unaoingia moyoni hauwezi kufa.Rachael Wandeto alikuja kimya, akaimba kwa nguvu, akaondoka ghafla. Sasa ni jukumu letu kuhakikisha wimbo wake hauzimi na yeye.

    Kwa sababu kama alisema mwenyewe katika wimbo wake wa mwisho kabla ya kufa:  “Wakiuzima mshumaa wangu, nitawaka kama jua.”

     

  • KIVULI CHA SIASA

    Na Chelangat Caren,

    Kenya, nchi ya jua na vivutio vya watalii, imekuwa ikisumbuliwa na siasa za kikabila kwa muda mrefu. Uchaguzi wa 2022 ulileta matumaini mapya ya mabadiliko, lakini sasa inaonekana kama siasa za kikabila zinarejea tena. Mgombano kati ya Rais William Ruto na Makamu wake wa zamani, Rigathi Gachagua, umefichua mgawanyiko wa kikabila ndani ya serikali .
    Siasa za Kenya zimekuwa na tabia ya kutumia lugha za chuki na mashambulio ya kibinafsi kama mbinu ya kushawishi wafuasi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha utulivu wa kisiasa nchini. Wataalamu wanasema kuwa siasa za Kenya zimekuwa zikiongozwa na maslahi ya kikabila, ambapo wanasiasa hutumia hisia za kikabila kuwashawishi wapigaji kura.
    Siasa za kikabila nchini Kenya si jambo jipya. Tangu uhuru, nchi imekuwa ikipitia misimu ya siasa za kikabila, ambazo zimepelekea machafuko na kifo cha watu wengi. Uchaguzi wa 2007 ni mfano wa jinsi siasa za kikabila zilivyokuwa na athari mbaya kwa nchi.
    Siasa za kikabila zina athari mbaya kwa nchi. Zinapelekea mgawanyiko wa kijamii, kuhatarisha mshikamano wa taifa, na kuzuia maendeleo ya nchi. Pia, zinaweza kusababisha machafuko na kifo cha watu wasiokuwa na hatia.
    Kuelekea uchaguzi wa 2027, ni muhimu kwa wanasiasa wa Kenya kuzingatia masuala ya kitaifa badala ya maslahi ya kikabila. Wananchi pia wanajukumu la kuchagua viongozi wanaotanguliza maendeleo ya nchi. Ni wakati wa Kenya kuachana na siasa za kikabila na kuzingatia maendeleo ya nchi.
    Wananchi wa Kenya wanajukumu kubwa katika kuamua mustakabali wa nchi yao. Ni muhimu kuchagua viongozi wanaotanguliza masuala ya kitaifa na kuacha siasa za kikabila. Pia, ni muhimu kushiriki katika mchakato wa kisiasa na katika uwajibikaji kutoka kwa viongozi.
    Siasa za kikabila nchini Kenya ni tatizo kubwa linalohitaji kushughulikiwa. Ni wakati wa wanasiasa kuzingatia masuala ya kitaifa na kuacha siasa za kikabila. Wananchi pia wanajukumu la kuchagua viongozi wanaotanguliza maendeleo ya nchi. Kenya inaweza kufikia maendeleo ikiwa itaachana na siasa za kikabila.
    Kenya inasimama kwenye kizingiti cha mabadiliko. Uchaguzi wa 2027 ni fursa ya kuandika upya mustakabali wa nchi. Wananchi wana uwezo wa kuchagua viongozi wanaotanguliza umoja na maendeleo, na kuacha siasa za kikabila nyuma. Je, Kenya itaamka na kupaa kama tai, au itaendelea kukumbatia kivuli cha mgawanyiko? Mustakabali ni wetu kuamua.

  • Vita vya Kutisha Sudan na Matokeo Yake

    Na Joe Aura, aurajoe6@gmail.com 

    Dunia iko wapi? Kwa nini msitusaidie? Hili ni swali la mama mmoja aliyenusurika katika machafuko ya Sudan, maneno aliyoyasema kwa majonzi huku machozi yakitiririka. Katika vita vya kuwania mamlaka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF), maisha ya mamilioni yamebadilika kwa njia zisizoelezeka, huku masuala muhimu yakiwa hayaripotiwi ipasavyo.

    Chanzo cha Mzozo

    Vita kati ya SAF na RSF vilianza Aprili 2023, vikisababisha vifo vya maelfu na kuwafurusha mamilioni ya watu kutoka makazi yao. Ingawa vyombo vya habari kama BBC Kiswahili vimeripoti matukio ya dhuluma kama ubakaji na ukatili, masuala mengine yanayochangia hali mbaya ya kibinadamu yameachwa bila kufafanuliwa kwa kina.

    Athari za Mazingira

    Ukame mkali na mafuriko hatari yameongeza changamoto kwa jamii za Sudan ambazo tayari zinakabiliwa na athari za vita. Mabadiliko ya tabianchi yanayozidi kuzorota yanasababisha uhaba wa maji na chakula, hali ambayo haizungumziwi kwa upana katika vyombo vya habari.

    Mgogoro wa Wakimbizi

    Zaidi ya watu milioni moja wamekimbilia Sudan Kusini, huku watu milioni 14 wakihamishwa ndani ya nchi. Maeneo yanayopokea wakimbizi yameelemewa na uhaba wa rasilimali, hali inayohitaji msaada wa dharura wa kimataifa.

    Changamoto za Misaada ya Kibinadamu

    Kupatikana kwa misaada ya kibinadamu ni changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa usalama na vikwazo vya usafiri. Mashirika ya misaada kama Shirika la Chakula Duniani (WFP) yamekuwa yakijitahidi kupenya katika maeneo yaliyoathirika zaidi, lakini juhudi zao zimegonga mwamba mara kwa mara.

    Njaa na Ukame

    Hali ya njaa imefikia kiwango cha janga, huku watu zaidi ya milioni 25 wakiwa na njaa kali. Katika kambi za wakimbizi na maeneo ya vijijini, watoto wanakufa kwa utapiamlo, hali ambayo ni ya kusikitisha na isiyofaa kupuuzwa.

    Ukatili wa Kijinsia

    Katika mizozo kama huu, wanawake na watoto wamekuwa wahanga wakuu wa unyanyasaji wa kijinsia. Ripoti kutoka kwa mashirika kama Amnesty International zinaonyesha kuwa ubakaji na dhuluma zimeongezeka kwa kasi, lakini simulizi hizi bado zinasikika kwa nadra kwenye vyombo vikuu vya habari.

    Athari kwa Elimu na Vijana

    Shule nyingi zimefungwa, na mamilioni ya watoto wa Sudan wameachwa bila elimu. Licha ya changamoto hizo, vijana wa Sudan wanaonyesha uvumilivu na matumaini, wakiwa tayari kujenga upya nchi yao ikiwa dunia itaonyesha mshikamano wa dhati.

    Huku dunia ikitazama, simulizi nyingi za mateso ya watu wa Sudan zinaendelea kuachwa bila kusikika. Ingawa vyombo vya habari kama BBC Kiswahili vimeangazia sehemu ya mzozo huu, masuala kama athari za mazingira, changamoto za misaada, na ukosefu wa elimu yanahitaji sauti zaidi. Kilio cha watu wa Sudan kinabaki kuwa kilio cha matumaini, wakitarajia msaada wa kimataifa utakapowafikia.

    Je, tutaendelea kufumbia macho hali hii au tutasikiliza kilio chao?

     

  • Mlipuko wa Virusi vya Marburg Nchini Tanzania

    Joe Aura, aurajoe6@gmail.com 

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza mlipuko wa virusi vya Marburg wiki moja tu baada ya waziri wa afya kukanusha uwepo wa visa vyovyote.

    Kisa cha kwanza kilichothibitishwa cha virusi vya Marburg kiliripotiwa katika mkoa wa Kagera, kaskazini-magharibi mwa nchi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu. Tangazo hili lilitolewa wiki moja baada ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, kukanusha uwepo wa virusi hivyo nchini. Rais Samia alihakikishia umma kuwa serikali imeimarisha juhudi za kukabiliana na mlipuko huo, ikiwa ni pamoja na kutuma timu ya dharura kufuatilia na kushughulikia visa vinavyoshukiwa.

    Tishio la Virusi vya Marburg

    Shirika la Afya Duniani (WHO) liliripoti awali mlipuko ulioshukiwa mnamo Januari 14, likisema kulikuwa na visa tisa na vifo vinane katika mkoa wa Kagera. Hata hivyo, uchambuzi wa sampuli ulibainisha kuwa ni kisa kimoja pekee kilichothibitishwa, huku visa vingine 24 vilivyoshukiwa vikipatikana kuwa hasi.

    Virusi vya Marburg, vinavyosambazwa kwa binadamu kupitia popo wa matunda na kwa kugusana na majimaji ya mwili ya watu walioambukizwa, ni hatari sana. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, kuhara, kutapika, na katika hali mbaya, kifo kutokana na kupoteza damu kupita kiasi. Kwa wastani, virusi hivi huua asilimia 50 ya walioambukizwa, ingawa hatari ya kimataifa inachukuliwa kuwa ya chini, kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus.

    Tanzania ilikumbwa na mlipuko wa Marburg hapo awali mnamo Machi 2023, ambao uliua watu sita katika wilaya ya Bukoba. Mlipuko wa sasa unasisitiza hitaji la ufuatiliaji madhubuti katika maeneo yenye hatari kubwa kama Kagera, ambayo ni kitovu cha usafiri kwa wasafiri kutoka nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Burundi, na Rwanda.

    Shirika la Afya la Umoja wa Afrika, Africa CDC, linaripoti zaidi ya watu 300 waliotambuliwa kwa uchunguzi, wakiwemo wafanyakazi wa afya 56. WHO inashauri kutozuia safari, ikisisitiza ushirikiano wa kimataifa ili kudhibiti mlipuko huo.

    Kenya Yachukua Hatua za Tahadhari

    Huku kisa cha Marburg kikithibitishwa Tanzania, Wizara ya Afya ya Kenya imeongeza umakini. Ingawa hakuna kisa chochote kilichoripotiwa Kenya, mamlaka zinaimarisha mifumo ya ufuatiliaji, kufanya tathmini ya utayari, na kuandaa mpango wa kina wa kukabiliana na ugonjwa wa Marburg (MVD). Wizara hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa vifaa vya kujikinga (PPE) kwa wafanyakazi wa afya na wale wanaowatunza wagonjwa ili kuzuia maambukizi.

    Kenya inabakia macho kutokana na mienendo mingi ya kuvuka mipaka na Tanzania, huku ikijitahidi kulinda afya ya umma dhidi ya MVD.

     

     

    Marejeo

    • BBC News; Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan athibitisha mlipuko wa virusi vya Marburg

    • Standard; Kenya yachukua tahadhari baada ya virusi vya Marburg kuthibitishwa Tanzania – The Standard Health

     

  • Hongera Septemba

    Na Mariita,

    Muhula wa Septemba umejawa na matukio mbalimbali ikiwemo michezo ya Falcon, burudani, wiki ya maonyesho ya mila na desturi za Kiafrika, biashara, utandawazi, mkutano wa kukuza mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa vilevile kuweka msingi wa ujenzi wa maskani ya wanachuo.

    Hatua hii muhimu ya kulishughulikia suala la maskani, imeibua hisia chanya kwani Naibu Chansela Prof. Ayiro na bodi ya chuo hiki, amefanikisha mchakato wa mradi huu kwa upesi. Kwingineko, mradi wa ujenzi wa Mama Musau- Shule ya Sheria, unazidi kunoga kwani ukitembea kwenye sehemu ya tukio la ufundi, utashibishwa na mizani ya waashi ilivyoimara. Ni wazi kwamba Imani ya wengi sasa imetiwa kwenye kiambo.

    Aidha, kuna hamu kubwa ya kutaka chuo hiki kuangazia mradi ambao wengi watauita ‘MAMA YAO’ kwani kiuhalisia, bila pingamizi na kwa ushawishi mkubwa; Chuo Cha Dayastar kinafahamika nchini na ukandani kama Chuo Cha Mawasiliano. Uvumi wa sifa zake ni kama mawimbi baharini, kuenea kwa ubora huu kumetikisa mashariki na kati. Kiukweli, shule ya mawasiliano imepeperusha bendera na kuwa kama kitambulisho kamili cha Chuo Cha Daystar.

    Kituo chetu cha Redio Ya Shine, mitabendi 99.9 kingali kinafanyiwa ukarabati na hayo ni maendeleo kwenye sekta ya mawasiliano. Zaidi, ingelikuwa bora mno ikiwa kituo cha televisheni, ambacho sio tu kwa kuleta programu mbalimbali zihusianazo na habari, burudani, kupeperusha ibada chuoni na matukio ya ukuaji, kingelipata sehemu mwafaka ambayo ni jengo la shule ya mawasiliano ili kufufua uwajibikaji kwa kutoa motisha na kuwapa kipaumbele wenye talanta mbalimbali.

    Safari ya maendeleo italazimu kila mmoja kujibidiisha ili kudumisha sura ya Chuo na maadili kama mojawapo ya changizo katika kuimarisha ubora wa masomo na uongozi tabithi. Muhula huu wa Septemba unazidi kufunua vyungu vya mabadiliko na vilevile kupekua kurasa za maendeleo mahali mahali.

     

  • STR8 UP YAALIKA KIZAZI CHA GEN Z

    Na Leeroy Wuone

    Wanafunzi wa chuo kikuu cha Daystar shule ya mawasiliano walihudhuria hafla iliyoandaliwa Standard group mnamo Jumamosi tarehe 28 Septemba mwaka wa 2024.Wanafunzi kumi na watatu walihudhuria hafla hio iliyobandikwa jina “Siku ya ubunifu ya kizazi cha Gen-Z’’.

    Lengo la Standard group la kuandaa hafla hio ilikuwa kuwahamasisha wanafunzi kuhusu mambo yanavyoendelea kwenye studio pale Standard group na ambavyo watu tofauti tofauti hushirikiana kila siku kuleta habari kemkem za hivi punde kila siku,zaidi ilikuwa siku ya kutangamana na wasanii kwenye sekta mbalimbali mfano ni anayejulikana kwa jina mluo_social.light ambaye alihudhuria hafla hiyo na kikosii chake ambao wametamba kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kama Instagram na Tiktok.

    Aliyetuzungusha kwenye sakafu ya kwanza “ red carpet’’ alisema kuwa uchapishaji wa magazeti ndio ulikuwa mwanzo wa the standard group kisha ikaja enzi ya televisheni na baadaye habari kwneye mitandao ya kijamii.

    Kelly alipeana mfano akisema kwamba tuseme iwapo mwanahabari ametumwa kule CBK kwenye hafla ya uchapishaji wa noti mpya hawezi kuiweka taarifa hio mtandaoni bila kuwajulisha wahariri ambao wako kwenye chumba cha habari.

    Kupangwa kwa red carpet ulikuwa kimkakati ndiposa waandishi wa habari hao waweze kufanya kazi kwa kijumla ili kushinda ushindani.Alitujulisha kuwa zile tahadhari za kwanza za habari hutumwa kwenye “radar desk’’ kwenye kituo cha Standard group. Lengo lao pia ni kulisambaza habari vilivyo bila kuutia chumvi .

    “Checkpoint’’ ilikuwa katikati na hapo ndipo habari za kiteknolojia kama kilimo na hata mambo ya takwimu yalifanyiwa utafiti kabla habari kupeperushwa.Mfano wa takwimu ni kwa mfano idadi ya magari ambayo Wakenya hununua na magari yapi kwa idadi?

    Iwapo mwanahabari ana tashwishi na utafiki wake ya nambari ataelekea kwa wanaofanya hapo checkpoint kwa usaidizi mwafaka. Alizidisha kwa kusema iwapo wanaofanya hapo checkpoint wapokee hadithi yako kama mwanahabari,wanaweza kupa takwimu zaidi ambayo ni sahihi mno.

    Mwanafunzi mmoja aliuliza kuhusu watu ambao wanaendesha tarakimu zilizoandikwa kwenye runinga pale kwenye red carpet kisha alijibu ya kwamba kuna wasanidi wa wavuti ama ukipenda kwa kiingereza “web developers’’ ambao kazi yao ni kujumuisha idadi ya Wakenya wanaosoma taarifa za magazeti kwa siku moja.

    Mwishowe wageni walitumbuizwa na hata kucheza densi. Watu waliweza kujifunza mengi na hata kujenga mahusiano na wakubwa katika sekta ya mawasiliano.

     

  • HEKAHEKA ZA MUHULA WA SEPTEMBA

    Na Mariita Joshua Ongoro

    Ni kweli kwamba mihula ya masomo hapa chuoni huwa na mambo yanayochipuka mwanzoni, kati na hata mwishoni. Muhula ukianza kawaida kuna kule kung’ang’ana na hali ya ulipaji karo, usajili wa masomo na mahudhurio ya mara kwa mara. Zaidi, hamna jambo linalobubujisha msongo wa mawazo kama vile kukosa chumba cha kupanga. Je, ni wangapi huzurura kotekote, mapana na marefu, kujaribisha nasibu ya kupanga angalau hata mabatini? Wakati mwingine huambulia patupu kwa kusononeshwa na kauli za wasimamizi wa vyumba vya kupanga, “Hamna chumba labda ujaribishe huko Portland.” Tabu. “ Ama kama hutojali, kunacho chumba pembeni kuleee… hakina umeme ila baadhi ya wenzenu wameshawahi kuishi siku za nyumba hali hii ilipojitokeza.” Utamsikia akiongeza kwa kutojali kana kwamba ni jeuri.

    Mbanano wa wanachuo nje ya shule imeleta hali chanya na pia hasi. Vyumba vya kupanga kila sehemu vimebeba mamia ya wanachuo na ni dhahiri kwamba wamiliki wa vyumba hivyo, hawajajutia ujenzi wao japo uliwagharimu kiasi kikubwa cha fedha. Kwa upande mwingine, uhitaji wa upangaji umeibua mijadala na hisia tofautitofauti kuhusu ongezo la kodi. Vyumba ni vile vile, hali ni ile ile, wanafunzi ni wale wale, maji ni yale yale tena ya chumvi; itakuwaje kuongeza kodi hata muda hamna vyumba vya kupanga? Sarakasi hii, pengine inawafaidi pakubwa wasimamizi hata kupita wamiliki halisi.

    Uhalisia wa elimu ya chuo inafafanuliwa kivipi? Je, kuna namna inayoweza kujitokeza ili iwe suluhisho kwa misukosuko na mawimbi ya jinsi hii? Cha kusikitisha ni kwamba, jinsi ujio wa wanachuo unazidi kunoga, basi hali hii inazidi kuyumbisha matamanio. Ingawaje kuna mahafali wa kila mwaka, wanaoingia huzidi mtoko. Sintofahamu inayopeperusha bendera miongoni mwa wanachuo ni kwamba chuo hiki, kwa jinsi kinavyofahamika kwa sifa zake, je, haingekuwa dhahiri kuwekeza katika miradi inayowanufaisha wanafunzi maana hawa ndio walengwa wakuu?

    Hatuwezi kulifumbia macho suala la Naibu Chansela, Prof. Ayiro kuchakatua miradi ya maendeleo kila baada ya muhula ama tuseme kila siku. Ni wazi bila pingamizi kuwa kati ya wazalendo na wachapakazi wa kweli, basi Profesa Ayiro amevikwa taji kwani ni mmoja wao na pengine kiongozi wao. Lakini mojawapo ya wasilisho la ombi kuu ambalo lingehitaji uchambuzi ni hili: Ujengaji wa vyumba vya malazi kwenye ardhi ya chuo hiki.

    Umuhimu wa ujenzi wa vyumba hivi ni pamoja na kodi inayoweza kugharamiwa na wanachuo hata wa kiwango cha chini. Ukengeufu uliopo kwenye mazingira ya nje ya shule ni pamoja na ukosefu wa maji, maji yasiyo safi kwa hali ya kutotibiwa mfano kwa njia ya klorini. Ukuaji wa chuo hiki kunategemewa na vizazi kwa sababu kutawafaidi waliomo na wasiokuwemo. Hivi sasa wanachuo wanazidi kukumbwa na hali ya kumudu maisha na pia utekelezaji wa majukumu yao kama vile kufika chuoni kwa wakati, kutimiza maono na lengo la elimu. Ladha ya kufanikisha vipengele vyote muhimu itatiwa kwa kulainishwa kwa masuala tata kama haya ya upungufu wa vyumba vya kupanga. Hekaheka za Septemba zahitaji hali kutengemaa.

  • Rais Ruto Awasimamisha Mawaziri Wote, Atangaza Mabadiliko Makubwa Serikalini

    By Joe Aura

    mawasiliano: aurajoe6@gmail.com

    {picha ya REUTERS}

     

    Nairobi, Kenya – Julai 11, 2024:

    Katika hatua muhimu, Rais William Ruto ametangaza mabadiliko makubwa katika utendaji wa serikali, akieleza haja ya kuwa na serikali nyembamba na yenye ufanisi ili
    kutimiza matarajio makubwa ya Wakenya.

    Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali imekuwa ikilenga Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi ya Chini Juu (BETA), jukwaa ambalo Rais Ruto alichaguliwa nalo katika Uchaguzi Mkuu wa 2022. “Tumepiga hatua kubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha uchumi, na kupunguza gharama ya maisha,” alisema Ruto, akisisitiza mafanikio muhimu kama vile kuimarisha bei za mafuta na kupunguza mfumuko wa bei.

    Sekta ya elimu imeona mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo yanayohusiana na Mtaala wa Msingi wa Ujuzi (CBC) na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu unaolenga wanafunzi. “Tumewaajiri walimu 56,000 kwa shule za msingi na sekondari na wakufunzi 2,000 kwa taasisi za Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET),” alisema Rais.

    Ruto pia alizungumzia maboresho katika ustawi wa jamii, hususan mpango wa uhawilishaji fedha kwaWakenya wanyonge. “Walengwa sasa wanapokea fedha zao sawia na mishahara ya watumishi wa umma,” alibainisha. Hazina ya Hustler, inayolenga kuongeza ushirikishwaji wa kifedha, imewasajili wakopaji milioni 22 na kuwaondoa Wakenya milioni 7 kwenye orodha ya Wakala wa Marejeleo ya Mikopo.

    Makazi na viwanda pia yamekuwa maeneo ya kipaumbele. “Mpango wetu wa Makazi Nafuu una zaidi ya vitengo 100,000 vya ujenzi kote nchini, ukiwaajiri vijana 160,000,” alitangaza Ruto. Aidha, ushuru uliowekwa kwenye uagizaji wa klinka na nondo umefufua viwanda vya ndani, kuokoa fedha za kigeni na kuunda ajira.

    Ajenda ya mabadiliko ya kidijitali inaendelea vizuri, na huduma 17,000 za serikali sasa zikiwa mtandaoni na vituo vya kidijitali 274 vikifanya kazi. Katika afya, waelimishaji afya wa jamii 107,000 wameajiriwa, na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii unatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 1, 2024.

    Katika hatua ya uamuzi, Rais Ruto amewafuta kazi Mawaziri wote na Mwanasheria Mkuu, isipokuwa Waziri Mkuu wa Baraza na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora. “Uamuzi huu unafuatia tathmini ya jumla ya utendaji wa Baraza langu la Mawaziri,” alieleza Ruto, akisisitiza haja ya kuwa na serikali ya upana ili kuharakisha mageuzi muhimu.

    Katika kipindi cha mpito, shughuli za serikali zitaendelea chini ya uongozi wa Makatibu Wakuu na maafisa wengine. “Nitaendelea na mashauriano ya kina kuunda serikali itakayoweza kushughulikia madeni, kuunda ajira, na kupambana na ufisadi kwa ufanisi,” alihitimisha Ruto.

    Hatua zaidi zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.

  • Kisanga cha Mlipuko wa Gesi

    Na Abdul Shaban

    Mlipuko wa gesi ulisababisha moto umeuwa watu wawili na kujeruhi zaidi ya 200 katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, mamlaka imesema leo.

    Mlipuko huo ulitokea katika mtaa wa Embakasi jijini Nairobi kabla ya saa sita usiku katika kampuni ya kujaza gesi, ambayo jengo lake liliharibiwa vibaya, msemaji wa serikali alisema.

    Moto huo uliteketeza ghala la nguo na lililokuwa karibu, huku ukiharibu magari kadhaa na mali za biashara na makazi, alisema.

    “Kutokana na hayo, Wakenya wenzao wawili wamepoteza maisha kwa masikitiko makubwa walipokuwa wakihudumiwa katika Hospitali ya Nairobi West,” alisema katika taarifa hiyo na kuongeza watu 222 walijeruhiwa katika tukio hilo.

    Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema vitengo mbalimbali vya dharura vimewalaza watu 271 katika hospitali za Nairobi.

  • TATANISHI LA MAFURIKO MJINI MOMBASA

     

    Na Ashley Mbashu

     

    Kulingana na taarifa za hali ya anga, sehemu tajika za kaunti ya Mombasa zimeshuhudia mvua ya  mno.

     

    Mafuriko yanaendelea kuzua misukosuko mjini Mombasa. Baadhi ya mikoa iliyoathirika kupita kiasi ni eneo la Bamburi, Old Town na kwingineko.

    Takwimu za serikali zinaarifu kuwa kaunti 33 zimeathirika kutokana na mvua kubwa

     

    Idadi ya vifo yasemekana kufika watu sitini na mmoja, wanane hawajulikani waliko,waliojeruhiwa 235  kutokana na mvua hiyo. Nyumba zilizoathirika ni 80518, biashara  143, vituo vya afya 25, vituo vya mifugo 11610,shule 10. Miongoni mwa walioripotiwa kupotea ni maafisa wawili wa halmashauri utozaji ushuru KRA, gari lao kusombwa na maji eneo la Ramisi katika Lungalunga walipokuwa wakisafiri kuelekea Mombasa.

     

    Serikali za kaunti zashauri walio maeneo hatari kuhamia maeneo salama. Hamasisho latolewa wenye magari kuwa waangalifu zaidi.