Use the link above to access the Involvement Newspaper issue 239 which features a range of articles written by our writers to ensure that you stay informed on News within and outside Daystar.
Use the link above to access the Involvement Newspaper issue 239 which features a range of articles written by our writers to ensure that you stay informed on News within and outside Daystar.
Na: Dorothy Waweru
dorothywaweru161706@daystar.ac.ke

Sikukuu ya Moi chuoni Daystar ilisherehekewa kwa mbwembwe, vifijo na nderemo kwani katika uga wa “Santiago Barna Betheli” kama unavyojulikana na wacheza kandanda wengi, mchuano mkubwa ulikuwa ukiendelea. Mchuano huo uliandaliwa na wanafunzi wacheza kandanda ikiwemo; Walter Nalwa, Nicholas Atulo Snr, Cedrick na Dadiseh Olwaga ambao walinuia kujiburudisha katika mchezo huo wa miguu.
Mchuano huo ulijumuisha timu sita zikiwemo: Blueboys, Rawa, Buffoons, Bomboclats, DCF handball na Fimbu. Timu hizi zilimenyana vilivyo ili kushinda zawadi murwa ambayo ilikuwa ni mbuzi mzima. Timu za Buffoons na Rawa ndizo zilifungua uga huo ambao ulikuwa na utelezi kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha usiku wote.
Timu ya Buffoons ilijikakamua katika dakika za kwanza huku Caleb Msando akiifungia timu hiyo bao la kwanza naye Nicholas Atulo Snr akifunga bao lao la pili. Timu ya Rawa ilijikakamua katika kipindi cha lala salama ambapo John Lemaiyan aliifungia Rawa bao lao la kwanza. Kitengo hicho cha kwanza cha mchezo kilipotamatika, Buffoons walikuwa wamefunga mabao mawili kwa moja.
Mashabiki wa timu ya Buffoons walijaa uwanjani wakiimba nyimbo za ushindi kwani timu hiyo ingemchinja mbuzi kama zawadi ya ufanisi wao iwapo wangewashinda wenzao kwenye semifinali. Baada ya dakika chache za mapumziko, timu ya DCF handball ilijitosa uwanjani kumenyana na wachezaji wa timu ya Fimbu. Uzoefu mkuu katika mpira wa mikono wa timu ya DCF handball ulionekana kuwapa mkono uwanjani. Hata hivyo baada ya dakika kumi na tano Wallace kutoka timu ya Fimbu alifunga bao la kwanza. Baada ya dakika zingine tano, DCF handball ilisawazisha kupitia mchezaji Ephantus.
Baada ya nusu wakati wa mchezo huo, timu ya Fimbu ilifunga bao lingine ambalo liliwawezesha kuibuka washindi katika kitengo hicho kwa mabao mawili kwa moja. Timu ya Blueboys vilevile ilichuana na timu ya Rawa huku wakifunga bao lao la kwanza ambalo lilikuwa la pekee katika mchezo huo hivi basi kuibuka washindi dhidi ya Rawa.
Hata ingawa jua lilikuwa mtikati, wachezaji wa Bomboclat waliingia ugani kumenyana na DCF handball. Yasemekana kuwa wachezaji wa Bomboclat walikuwa wamekesha wakijitayarisha kwa mchuano huo wa kipekee. Katika dakika za kwanza, Bomboclat ilifunga bao lao la kwanza na baadaye kufunga la pili. DCF handball ilijizolea nunge hivi basi Bomboclat kuibuka washindi.
Isitoshe, kabla ya semi fainali, Bomboclat ilichuana na Fimbu na wakailaza Fimbu bao moja kwa nunge. Timu zilizofuzu kwenye semi fainali ni Fimbu, Buffoons, Bomboclat na Blueboys. Mechi ya kwanza katika semi fainali ilikuwa kati ya Buffoons na Fimbu. Buffoons walilazwa bao moja la kufunga virago baada ya kucheza kwa ukakamavu mwingi sana.
Nyuso za wachezaji wa timu ya Buffoons zilijaa simanzi kwani mbuzi alikuwa amewakwepa. Lisilobudi hubidi, Buffoons walidondolewa kwenye mchuano wakabaki kuwa mashabiki tu. “Ni uchungu sana mama kubeba mimba tumboni kwa miezi tisa halafu anampoteza mwana wake. Nasikitika sana kuwa tumeshindwa,” Duncan Olile, kipa wa timu ya Buffoons alisema.
Timu za Bomboclat na Blueboys zilichuana kwenye mchezo wa pili katika semi fainali huku Bomboclat ikiibuka mshindi baada ya kuilaza Blueboys mabao mawili kwa nunge. Washindi wa semi fainali walikuwa Bomboclat na Fimbu. Wakati ukiwa saa kumi na mbili kamili, mchuano kati ya timu hizi mbili ulianza huku Bomboclat ikifunga mabao mawili mida ya dakika za kumi na tano za kwanza. Japo Fimbu iling’ang’ana kiudi na uvumba kujizolea angalau bao moja, jitihada zao hazikuzaa matunda kwani katika kipindi cha pili cha mchezo huo, Bomboclat ilifunga bao lingine. Bomboclat wakafunga mabao matatu kwa nunge.
Mbwembwe na shamrashamra zilijaa uwanjani wakati ambapo wachezaji wa Bomboclat walipokabidhiwa mbuzi wao. Wachezaji waliachwa ugani wakisherehekea ushindi wao huku mashabiki wakiungana nao kushangilia ushindi wao.

Na: Dorothy Waweru
dorothywaweru161706@daystar.ac.ke
Picha kwa hisani ya: The Star
Ni afueni kwa wakenya wote na haswa familia yake Bi. Mariam Kighenda kwa kutolewa katika hindi la Victoria.
Shughuli hii iliyochukua siku kumi na tatu, imezifanya nyoyo nyingi sasa kupata na utulivu. Aila ya Bi. Mariam sasa inauhuru wa kuzipumzisha mili ya wapenda wao ambao wamesumbuka usiku kucha. Japo bado uchungu upo, tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho zao pahala pema peponi.
Hata hivyo, Shirika la Kenya Ferry limekabiliwa na mashtaka chungu nzima kufuatia ajali iliyotokea katika kivuko cha Likoni. Ajali hiyo ilihusisha kutumbukia kwa gari moja kwenye bahari hindi mnamo Septemba ishirini na tisa mida ya saa kumi na mbili. Gari hilo lilikuwa na abiria wawili, Bi. Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu.
Yasemekana wawili hawa walikuwa wametoka kuzuru shamba katika kaunti ya Kwale na walikuwa wakirejea nyumbani walipopatana na kifo chao.
Matukio yaliyojiri baadaye yanaashiria utepetevu mkuu wa shirika la Kenya Ferry katika kutekeleza majukumu yao ya kuhakikisha usalama wa wasafiri.
Baada ya ajali hiyo kutokea siku ya Jumatatu tarehe thelathini Septemba, Kenya Ferry kupitia mtandao wa kijamii wa twitter ilitangaza kuwa watahakikisha kuna meli nne katika kivukio cha Likoni.
Wakenya kupitia mtandao huo walituma jumbe zilizosheheni kughadhabishwa kwa usemi wa Kenya Ferry kwani la muhimu lilikuwa kuomba msamaha kwa familia ya walioadhirika badala ya kuwaambia wananchi kuwa feri nne zitatutumika kuwasafirisha abiria hapo likoni.
Ni jambo la kukereketa maini kugundua kwamba shirika la feri halina mikakati bomba inayowahakikishia abiria usalama wao hasa wakati kuna tukio kama hilo linalohatarisha maisha yao.
Uchunguzi ambao unaendelea kufanywa umebaini kwamba shirika la feri la humu nchini halina wapiga mbizi ambao wanasafiri katika feri mchana na usiku bali wanawategemea wapiga mbizi katika shirika la Kenya Ports Authority na jeshi la baharini humu nchini.
Uhai wa mama Amanda na mwanawe haungekatizwa ghafla iwapo shirika la Kenya Ferry lingekuwa na wapiga mbizi katika chombo hicho wakati wa mkasa huo. Wapiga mbizi wangelikuwepo wangefanya hima kuwaokoa abiria hawa punde tu gari lao lilipoanza kuzama.
Msemaji wa serikali Col Rtd, Cyrus Oguna alipokuwa akitoa taarifa aliwaambia wanahabari kuwa gari lilichukua chini ya dakika moja unusu kuzama kwa hivyo kulikuwa na muda tosha wa kuwaokoa wasafiri hawa.
Sababu za kucheleweshwa kwa kutolewa kwa miili ya walioaga ni kuwa kuna meli zinazopita baharini kupitia bandari ya Mombasa kufanya biashara ambayo inailetea kaunti ya Mombasa fedha nyingi. Tunaelewa kwamba tukikatiza usafiri wa meli baharini uchumi wa Mombasa utaadhirika pakubwa.
Sababu ya pili ni giza kali ambayo imeshuhudiwa baharini hivyo wapiga mbizi wanatatizika sana. Tatu ni mawimbi makali yanayovuma baharini hivyo shughuli za uokoaji zinagonga mwamba wakati huo hadi mawimbi yatulie. Lakini ile sababu muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa usalama wa wapiga mbizi na wale wote wanaohusika katika shughuli za uokoaji unadumishwa,” haya yalikuwa maoni ya msemaji wa serikali Col Rtd.Cyrus Oguna.
Shirika la Kenya Ferry limeshuhudia visa kama hivi vya ajali bali ni hatua chache sasa zimechukuliwa kuimarisha utendakazi wao. Wasafiri hawana uhakika wa usalama wao kwani janga kama hili linaweza kutokea bila usaidizi wowote. Ni bayana kuwa uwepo wa kuwa tayari kukabiliana na mikasa ya baharini ni jambo linalofaa kutiliwa mkazo.
Feri zote zinafaa kuwa na vyombo vya kuhakikisha usalama wa wasafiri na magari pia. Sheria mpya zinafaa kubuniwa ili kuwe na mpangilio katika feri hizi. Hakuna mtu ambaye anafaa kupoteza maisha yake kupitia kisa cha kuhuzunisha kama hiki.

Picha kwa hisani ya: citizentv.co.ke
Na Gladys Sheila
gladyshila52@gmail.com
Picha kwa hisani ya: Joseph Gichari
Josephndungo55@gmail.com
Klabu ya Daystar Compassion and Care Center (DCCC) almarufu DC3 iliyoko katika chuo kikuu cha Daystar ilisherehekea uongozi upya. DC3, ni klabu ambayo imekuwepo tangu mwaka wa (2013) huku lengo lake kuu likiwa kufahamisha wanadaystar kuhusu maswala ya afya, kuwasaidia kisaikolojia wanafunzi, wahadhiri, wafanyakazi na jamii ya Daystar kwa ujumla. Klabu hii imekuwa chini ya uongozi wa Bi.Susan Botto ambaye ndiye mratibu wake.
Siku hii ya ndovu kumla mwanawe, iliyoadhimishwa katika chapeli iliwaorodhesha viongozi wake wa mwaka wa 2019-2020 huku waliowatangulia wakiwakabidhi faili za utendakazi wao. Siku hiyo ya aina yake ilianzishwa kwa tenzi za kumsifu na kumuabudu Mungu, hafla iliyoongozwa na kwaya ya Imela katika chuo kikuu cha Daystar. Hali kadhalika, wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi chuoni Daystar walipokea pipi huku ikiwa kiishara kuwa wasiokwenye ndoa wajihifadhi mpaka wakati wa kufunga ndoa.
Kilele cha hafla hii ni ufahamu dhabiti wa klabu hicho na wanajopo ambao walikuwa Bi. Emmah Nguli na Bwana Allan Ball ambao ni washauri wa maswala ya saikolojia.
Matayarisho ya siku hii isitoshe hung’oa habta wiki ikianza huku mada kuu ikiwa kuwahamasisha wanadaystar kufahamu afya zao. DC3 hukakisha kuna vitengo mbalimbali ambavyo vyaweza kuwasaidia kutambua hali zao za kiafya ikiwa upimaji wa ongoezeko au upungufu wa sukari mwilini, uchunguzi wa saratani, kuangaliwa meno na upimaji wa ukimwi. Ukabidhishaji wa nyara kutoka kwa naibu wa msimamizi mkuu wa wanafunzi Bi. Irene Kimani.
Waliotuzwa walikuwa:
1. David Obong’o- Rais
2. Gladys Sheila- Naibu wa Rais
3. Wilbert Kiprop- Katibu
4. Kevin Korir- Mweka Hazina
5. Maureen Minus- Mkurungezi wa Halfa
6. Chris Waweru- Msaidizi wa Vikundi vya Msaada
Erick Spira, rais anayeshika timu hiyo mpya mkono, aliwapongeza waliomtangulia na kuwahamasisha wanafunzi kuridhika kwa kasoro wanazojua wanazo kwani zina manufaa maishani. Kwa kuwa chanzo cha jambo ni mwisho wa kingine, timu hiyo ilijumuika na kukata keki ya kusherehekea uongozi upya na uliopita katika ofisi zao za DCCC.
Kweli sote kama wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi twawatakia viongozi hao kila la heri wanapoongoza wanadaystar.








Na: Wangu Kanuri
kanuriwangu@gmail.com

Melina Gold, mwanzilishi wa begi za Melina Gold.
TUELEZE kuhusu ushoni wako wa mikoba [UTANGULIZI]
Mikoba ya Melina Gold, ninashona kwa kutumia ngozi. Utengenezaji wa mikoba hii ilianza mwaka wa 2019 Februari huku lengo langu likiwa kuutuza usanii na upekee wa vitu vya Kenya. Ushonaji wa mikoba hii hutumia ngozi na mshoni wangu ndiye hukarabati usanii kadha wa kadha.
TUELEZE kwa ufupi kukuhusu
Jina langu ni Melina Gold na mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo kikuu cha Daystar. Ninafanya shahada yangu katika mawasiliano kitengo cha uhusiano wa umma na nyongeza ya masomo katika saikolojia.
NINI kilikuchochea kuupenda kushona mikoba?
Ushoni wangu unanuia kuhamasisha wakenya kupenda na kuonea fahari mikoba ya Kenya kwa hivyo nikachukua jukumu hili kuzitengeneza mikoba ambayo itafifisha uduni wa bidhaa za Kenya. Hali kadhalika, nilitaka kuwazindua wanabiashara kujikita katika utengenezaji wa mikoba ili kuongeza mikoba yenye asili ya Kenya kwenye soko.
NI changamoto zipi unakumbana nazo katika ushoni huu?
Kutompata mshoni ambaye amebobea katika ushoni, kutowajibika kwa washoni ambao aghalabu hutumia ngozi hii kushona bidhaa nyingine zao bali si mikoba yangu, kutopata ngozi hii ya kutumia katika ushoni na kutopata watu ambao wanamaono sawa na yangu katika utengenezaji huu wa mikoba.
MIKOBA yako ni ya aina gani?
Melina Gold ni mikoba ambayo hutumia ngozi.
UNAWASHAURI vipi wanabiashara chipukizi?
Wasitegemee wanadamu kwani aliyemfunza chui kumla binadamu ni mtu. Pili waangaze maono yao kwa kina na wasiangeme. Mwisho wawe wenye bidii katika kuhakikisha biashara zao zimekua.
Wasiliana na Melina Gold Kupitia:
+254706602386
@melinagoldbagline on instagram





Na: Wangu Kanuri
kanuriwangu@gmail.com
TOA maelezo yako kuhusu mchezo wa raga
Raga ni mchezo ambao unahitaji nguvu haswa kwenye misuli. Mchezo huu umegawanywa katika makundi mawili makuu; ya wachezaji saba na ya wachezaji kumi na tano. Kundi hili la wachezaji saba hujulikana vyema kama rugby 7s ilhali hilo la wachezaji kumi na tano hujulikana kama rugby 15s. Vikundi hivi ndivyo vimepewa kipaumbele nchini ila kuna vingine.
TUELEZE kwa ufupi kukuhusu
Slyvester Miheso, ni mwanafunzi wa shahada ya Udhibitishaji wa Rasilimali za Nchi katika chuo kikuu cha Daystar. Anapenda kusikiza muziki, kufanya mazoezi na kutizama filamu. Isitoshe, mimi ni mchezaji wa kawaida katika timu ya Falcons ambayo ni timu ya raga katika chuo kikuu cha Daystar.
NINI kilikuchochea kuupenda mchezo huu wa raga?
Nilipojiunga na shule ya upili ya Mtakatifu Inyasi ndipo ari yangu ya kupenda mchezo wa raga ilianza. Nilijiunga na timu ya raga nikiwa kidato cha kwanza japo shingo upande kwa kuogopa kuumizwa. Baada ya kujiunga na mchezo huo nilijua sheria na masharti zinazomkinga mtu wakati wa kumenyana na hofu yangu ikapungua.
NI mchezaji yupi katika raga hukuvutia? Kwa nini?
Mchezaji ninayemuenzi anachezea timu ya na Mwamba anafahamika kama Collins Injera. Mchezaji huyu ana bidii na anapenda kuwapa mwelekeo wachezaji chipukizi ili waweze kubobea kama yeye. Isitoshe, Collins amejivunia taji nyingi katika ligi za Uingereza kwa kufunga mabao mengi.
MCHEZO HUU umekuvunia tija ipi?
Mchezo huu umeniwezesha kufadhiliwa kimasomo katika ya shule ya upili na ya chuo kikuu. Hali kadhalika, nimejivunia taji la mchezaji bora na pia mchezaji aliyefunga mabao mengi upande wa Division 2. Nimeweza kuzuru nchi ya Uganda na Rwanda na miji ya Kisumu, Kakamega, Nairobi, Meru, Nanyuki na Nakuru.
UNAWASHAURI vipi wachezaji chipukizi?
Wasififishe talanta zao kwani ni zawadi kutoka Maulana. Pili, wafanye bidii wakati wa mazoezi huku wakiamini wao ni wachezaji bora kwani jambo huanzia kwa kukata shauri akilini. Tatu, wasikate tamaa hata wakishindwa kwani kufeli si kujaribu bali kutojaribu.

wangukanuri181152@daystar.ac.ke
Na: Wangu Kanuri
Ilikuwa vuta nikuvute katika barabara ya Magadi baina wanafunzi wa chuo kikuu cha Multimedia na polisi. Wanafunzi wa chuo kikuu hicho waliandamana na kufunga barabara hiyo kufuatia ajali iliyomlaza mmoja wao katika hospitali kuu ya Kenyatta huku akiwa katika hali mahututi. Kamanda wa Langata bwana Gregory Mutiso aliwarai wasafiri kutumia njia mbadala wanapowatuliza wanafunzi hao waliokuwa wamekabwa koo. Ajali katika barabara hiyo zinazotamatisha maisha ya wanafunzi katika chuo kikuu hicho si jambo geni ndio maana maandamano hayo yaliyoonyesha kughadhabishwa kwa wanafunzi na madereva.
Kwa kutaka kuchukulia haki mikononi mwao kwa mwanafunzi huyo aliye katika mwaka wake wa kwanza na ambaye wiki jana aligongwa na yu katika hali mahututi, wanafunzi hao waliokerwa walistahimili vitoa machozi ambavyo maaskari waliwarushia nao wakiwarushia mawe. Mwanafunzi huyo aligongwa na matatu iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi mno hapo karibu na lango la chuo hicho kikuu. Isitoshe wanafunzi hao walilalamikia polisi kwa kuchelewa kushughulika baada ya mwanafunzi huyo kugongwa.
Uchungu uliokuwa nyoyoni mwa wanafunzi hao ulidhibitisha kuwa walikuwa wamekerwa na ajali zinazofanyika katika barabara hiyo zinazotamatisha nyoyo za wenzao huku wakikumbuka kuwa mwaka wa 2016 walipoteza wanafunzi wawili katika barabara iyo hiyo. Zaidi ya hayo, walilalamikia kuongezewa kwa nauli kwa matatu ya tume ya Ongataline na kunyanyaswa na waendeshaji wa magari hayo.
Japo gari hiyo iliyomgonga mwanafunzi hiyo I katika kituo cha polisi, usakaji wa dereva huyo aliyemgonga mwanafunzi huyo bado waendelea. Hali kadhalika wanafunzi watatu walikamatwa katika maandamano hayo.