Category: Maoni

  • Umuhimu wa Kujifunza Lugha za Kienyeji

    Na Chelangat Caren chelangatcaren756@gmail.com,

     

    Katika ulimwengu wa leo, ambapo mawasiliano na teknolojia zimeendelea kwa kasi kubwa, lugha za kienyeji zimekuwa zikipoteza umaarufu na umuhimu wake katika jamii. Wazazi wengi wanapendelea watoto wao kujifunza lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kifaransa, au Kichina, wakiamini kuwa hizi ndizo lugha zitakazowasaidia watoto wao kufanikiwa katika maisha yao ya baadaye. Lakini je, tumewahi kufikiria umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza lugha zetu za kienyeji?

    Lugha ni sehemu muhimu ya utamaduni na utambulisho wa jamii yoyote. Kujifunza lugha ya kienyeji ni kujifunza kuhusu historia, mila, na desturi za jamii husika. Lugha za kienyeji ni hazina ya thamani kubwa inayopaswa  kuhifadhiwa na kupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

    Katika nchi nyingi za Kiafrika, lugha za kienyeji ni nyingi na tofauti, na kila moja ina historia na utamaduni wake wa kipekee. Kwa mfano, nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha ya taifa na inaunganisha watu wa makabila tofauti. Lakini zaidi ya Kiswahili, kuna lugha nyingine nyingi za kienyeji kama vile Kikuyu, Kinyakyusa, na Kimakonde, kila moja ikiwa na utajiri wake wa kipekee.

    Kujifunza lugha za kienyeji kuna faida nyingi. Kwanza, kunasaidia kuimarisha utambulisho wa kitamaduni na kukuza fahari ya asili yetu. Pili, lugha za kienyeji ni chombo muhimu cha mawasiliano katika jamii, na watu wanaozijua wanaweza kuwasiliana kwa ufanisi zaidi na wanajamii wao. Tatu, lugha za kienyeji ni hazina ya maarifa na historia ambayo inaweza kupotea kama hatutaichukulia kwa umakini.

    Hata hivyo, lugha za kienyeji ziko hatarini kutoweka kutokana na ushawishi wa lugha za kigeni na ukosefu wa matumizi yake katika mazingira rasmi na elimu. Serikali na taasisi za elimu zina wajibu wa kuhamasisha na kuendeleza matumizi ya lugha za kienyeji katika shule na mazingira ya kazi.

    Kama jamii, tunapaswa kutambua thamani ya lugha zetu za kienyeji na kuhamasisha watoto wetu kuzijifunza na kuzitumia. Tunaweza kufanya hivi kwa kuwahamasisha watoto kusoma vitabu vya Kiswahili na lugha nyingine za kienyeji, kuwasikiliza wanamuziki wanaotunga nyimbo katika lugha za kienyeji, na kushiriki katika shughuli za kitamaduni zinazotumia lugha hizo.

    Lugha za kienyeji ni sehemu muhimu ya utamaduni na utambulisho wetu. Ni vyema tukazipa thamani na umuhimu unaostahili, na kuhakikisha kuwa zinapitishwa kwa vizazi vijavyo. Tuendelee kuzihifadhi na kuzitumia lugha zetu za kienyeji kwa fahari na heshima.

  • TABIA NCHI

    {Picha kwa hisani ya As You Know}

                                                   

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com}

    Tabianchi ni hali ya mabadiliko ya mazingira ya hali ya hewa ikiwemo joto, mvua na pepo. Mabadiliko ya tabianchi yanapojitokeza kunaweza kutokea ongezeko la mawimbi ya joto, mizozo ya kimataifa, mafuriko na ukame unaoathiri viumbe hai.

    Kwa asilimia kubwa, mabadiliko haya yanachangiwa na shughuli za binadamu ikiwemo uchomaji wa makaa na mafuta katika viwanda, vituo vya umeme na kwenye magari.

    Ongezeko la joto linaweza kuleta athari kama vile; viwango vya maji baharini kupanda, bahari kuchemka na kuwa na tindikali zaidi, barafu vya vilele vya milima kuyeyuka na kusababisha mafuriko, kubadilika kwa mikondo ya bahari, ukosefu wa mvua itakayosababisha njaa na uhaba wa maji, ongezeko la halijoto, upepo, tufani na kuenea kwa magonjwa. Zaidi ya hayo, madhara haya yanaweza kusababisha vifo vya watu na viumbe hai kama mimea na wanyama na kuvifanya kutoweka.

    Janga hili la ongezeko la joto linaweza kuepukika ikiwa watu watachukua hatua ya kupanda miti, kupunguza kiwango cha utoaji wa hewa chafu ya kaboni, kukabiliana na matatizo ya taka yanayojikusanya kwenye mito na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

    Kando na hayo, watu wanaweza pia kujenga nyumba zinazoweza kumiliki mabadiliko ya tabianchi ili kuwa salama. Njia hizi ikiwemo kujenga kwa kuzingatia ukame, viwango vya joto, mafuriko, baridi, vimbunga na upepo mkali.

    Tunatakiwa kuhamisha uwekezaji wetu kutoka kwenye uchumi mchafu kuenda kwenye uchumi msafi unaotumia teknolojia inayowafikia watu wote katika nchi zote.

  •   BIASHARA YA OMBAOMBA

    {Picha kwa hisani ya Mwananchi}

     

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com} 

    Tumekua tukiona watu ikiwemo watoto na wazee walemavu barabarani wakiombaomba ili waweze kujikimu kimaisha. Ila cha kushangaza ni kwamba wengi wao wapo kibiashara, na sio tu biashara ya kawaida ila ni ile ya kutumikishwa.

    Baadhi ya watu hawa wanageuza kuwa mtaji, na nyuma yao ni watu wenye uwezo wanaowatumia ili kunufaika na kufaidi hizo hela au msaada unaotolewa kwa watu hawa. Kisichoaminika ni kua pesa hizo hupitia hesabu ya hali ya juu kama tu mapato mengine. Walemavu wengi hulazimishwa kutimiza matakwa ya waajiri wao ingawa hawaipendi kazi hiyo, kwani “Lisilo budi hutendwa.” Wengine wao wanahadaiwa kua wanatajirika katika biashara hio lakini mwishowe wanateswa, kunyanyaswa na kulipwa kiasi kidogo kisichowatosha.

    Changamoto inatokea pale mtu anapotaka kuwasaidia watu hawa wasiojiweza, anashindwa kujua nia ya kweli ya watu hao wanaohitaji msaada, kumbe wapo hapo kwa kulazimishwa.

    Watoto walemavu pia wanalazimishwa kuomba mitaani na wasipoleta pesa hua wanapigwa. Familia nyingi zinadanganywa kuwatoa watoto wao na kuenda kufanyishwa biashara ya kikatili na haramu. Watoto hawa wanasafirishwa na kuletwa kuja kutumikishwa mbali na wazazi wao na kulamishwa kukatika mawasiliano na wao.

    Kwa watoto wanaotumikishwa, imegundulika kua chanzo ni malezi. Wazazi au walezi wanadanganywa watoe watoto walemavu na kupewa ahadi kua watapewa misaada ya kifedha kama malipo yao ilhali watoto hao wanaenda kuteswa. Wazazi na walezi hawa wanatakiwa kuzingatia malezi ya watoto wao walemavu na kuhakikisha hawakati  tamaa kwa watoto hao na badala yake kuwalinda ili kuepukana na mazingira hatarishi. Jamii pia inatakiwa kuhakikisha kwamba watoto hawa walemavu wanalindwa ili wawe raia wema na sio mzigo kwa Taifa. Sio watoto tu, hata wazee walemavu wanahitaji ulinzi kwa sababu wanyanyasaji hawa wananufaika wakijua watu hawa wenye ulemavu hawajiwezi na wengine wametelekezwa.

    Hata hivyo, mbali na hawa wasiojiweza kutumikishwa, kuna walemavu, wanaofanya ajira hii kwa hiari kutokana na hali yao ya maisha kua ngumu, na hio ndio njia pekee itakayowawezesha kuishi na kutunza familia zao kwa wale wenye watoto. Wamama wenye watoto walemmavu au wamama mlemavu wenye watoto na wameachwa na waume zao kutokana na hali yao, huteseka sana. Walemavu hawa wanakubali kutumiwa kama vitega uchumu ingawa ni kwa mateso, kwani kwao “heri nusu shari kuliko shari kamili”.

    Hali nyingine ni ya ombaomba tapeli, ambayo pia ni biashara inayofanywa na baadhi ya watu wanaojifanya walemavu wakiombaomba ilhali si walemavu bali ni matapeli. Watu hawa wameamua kuanza biashara hii kwani wanaamini kuwa watu huwasaidia au kuwapa fedha watu wenye ulemavu tu. Mwisho wa siku, utawaona watu hawa wakielekea nyumbani bila ulemavu wowote, baada ya kuvuna ambapo hawakupanda.

    Watu hawa utawaona wakitambaa barabarani wakiwa wamevaa mavazi yaliyochakaa kabisa ili watu wengine waamini kuwa hawajiwezi. Kuna baadhi yao pia hukodisha watoto wao au wa ndugu na kuwatumia kama kitega uchumu ili tu wahurumiwe na kuchangiwa pesa. Wengi wao hutumia usafiri wa bodaboda ili wasionekane au kujulikana na watu.

    Biashara hizi za ombomba ni kinyume na sheria kwani inawazuia watu wenye ulemavu kutopata msaada kwasababu ya uoga uliojawa watu ya kuwa wanatapeliwa. Wapita njia wengi na hata waendesha magari wamepunguza kiasi cha kuwasaidia ombaomba barabarani kwa sababu wengi wao hawana ulemavu na hawaaminiki.

    Serikali inatakiwa kuwasaidia walemavu hawa na kuwashika hao matapeli  wanaojifanya.

  •  MFANYAKAZI WA NYUMBANI

    {Picha kwa hisani ya Conde Nast Travelers}

     

    Na: Gertrude Prosper

    {getrude2003@gmail.com}

    Kwa miaka mingi sasa watu wengi wamezoea kuwaajiri wafanyakazi wa ndani ili kuwasaidia kazi. Wafanyakazi hawa wa nyumbani ni wasaidizi au wakelezaji wa kazi zote za nyumbani ikiwemo kufua, kupika, kufanya usafi wa nyumba na mazingira, kuosha vyombo na baadhi ya kazi zingine nyingi wanazopewa na waajiri wao. Mbali na kazi hizo, wafanya kazi wengi hupewa kazi ya kulea watoto endepo mama au wazazi ameenda kazini, au kama wanataka kuendelea na shughuli zingine.

    Kabla sijaelezea jinsi baadhi ya mambo ya ajabu ambayo wafanyakazi huwafanyia watoto, tutaanza na jinsi wafanyakazi hawa huteswa katika baadhi ya sehemu wanapoajiriwa. Kwanza kabisa, mtu anapomwajiri mfanya kazi anatakiwa ahakikishe kua hamtesi wala kumyanyasa kwa namna yoyote ile, na badala yake anatakiwa akumbuke haki yake. Hii ni kwasababu wafanyakazi hawa ndio walinzi wa nyumba na wana uwezo wa kuiangamiza au kuistawisha familia.

    Wafanyakazi hawa hupitia changamoto nyingi kama vile kunyimwa chakula na mavazi mazuri, kupigwa, kutopewa mahali pazuri pa kulala, kufanyishwa kazi nyingi nje ya uwezo wao na hata kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao. Waajiri hawa husahau mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi hawa ingawa bado wanawahitaji.

    Kumetokea kesi nyingi ya wafanyakazi hawa wa ndani wa kike, kubakwa au kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao wakiume na hii imeleta migogoro katika familia nyingi na kusababisha kuvunjika kwa ndoa. Wengi wao wakitoa malalamiko, hawaaminiwi kwa sababu wanalaumiwa kuwa sababu ya kilichowapata. Unapata mume au baba mwenye nyumba ana familia ya pili na mfanya kazi wa ndani.

    Kuna baadhi ya haki ambazo wafanya kazi wanastahili kupewa ikiwemo likizo kwa sababu wengi wao hufanya kila siku bila kupumzika na inawalazimu kusingizia kuumwa ili waweze kupumzika au kuenda kuwasalimia wazazi wao nyumbani. Wanatakiwa pia walipwe mishahara yao kamili na kwa wakati, na kuhakikisha ulinzi wa afya na usalama wao.

    Kati ya hayo machache kuhusu haki na usalama wa wafanya kazi wa nyumbani, tutaangazia vitendo vya ajabu vinayofanywa na wafanyakazi hawa katika familia tofauti haswa kwa watoto wanaoachiwa kuwalea.

    Wafanya kazi hawa wa ndani hushikwa wakiwadhulumu, kushiriki kingono na watoto wa waajiri wao na wakati mwingine kuwapiga na kuwaumiza watoto hawa. Inasikitisha kwa sababu watoto hawa hushindwa kutoa mashtaka kwa wazazi kutokana na umri wao kua mdogo na sababu nyingine ni vitisho wanavyopewa. Wafanya kazi wengi hunyanyasa watoto kwa sababu ya kukosa subira pindi mtoto anapokataa kula, kulala au kumsikiliza.

    Wazazi hawa hugundua hizi shida na mateso watoto wao wanayoyapitia baadae sana wakati mtoto ashaharibiwa kupitiliza. Kesi nyingi zimetolewa dhidi ya wafanya kazi wa nyumbani lakini bado idadi inatia shaka. Wazazi wanatakiwa wahakikishe wanawaajiri wafanyakazi wazuri waliobobea ili watoto wao wawe kwenye mikono salama, kwa sababu wakati mwingi wapo kazini na wanachelewa kurudi hivyo hawajui kinachoendelea nyumbani. Wakati mwingine wazazi hawa wanashauriwa angalau kukaa na mtoto kwa muda mwingi na sio tu kutokomea kazini ilhali mtoto hayupo salama.

    Kutokana na uzoefu wa kuwaachia wafanya kazi wa nyumbani watoto ili wawalee, hamna namna nyingine bali kuhakikisha wafanya kazi hawa ni wa kuaminika na wenye utu na huruma.